Dk Mwinyi: Ichagueni CCM, tutajenga uchumi imara, kuvutia wawekezaji

Unguja. Siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzindua kampeni zake, mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Dk Hussein Mwinyi, amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini na wazee wastaafu wa chama na Serikali, kuwaomba kuendelea kuombea amani ili uchaguzi upite kwa usalama bila mifarakano.

Dk Mwinyi amekutana na makundi hayo leo, Septemba 14, 2025, katika ukumbi wa Abduwakil, Unguja, Zanzibar.

Amesema wakati wa kampeni za mwaka 2020 alikutana na viongozi hao lengo likiwa ni kuombea nchi amani, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo akaona ni vyema tena, anapomaliza awamu ya kwanza na kuanza safari ya awamu ya pili, kukutana nao tena ili kuwaomba waendeleze kuombea nchi amani izidi kutamalaki.

“Kwa sasa tulipo tofauti na tulipokuwa wakati tunaingia madarakani, watu hapa walikuwa hawasalimiani, waligawanyika, walikimbia misikitini, ndoa zilivunjika kisa utofauti wa kisiasa, lakini leo tunaona hakuna mambo kama haya.

“Kw ahiyo tumeona tuje tena tunapoanza safari hii, tuwaombe muendelee kuombea amani tuvuke salama,” amesema Dk Mwinyi.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, iwapo nchi ikiwa na amani, maendeleo ya nchi yatapaa mara dufu kama mipango yao inavyosema kuendelea kujenga uchumi imara, kuwavutia wawekezaji zaidi.

Mbali na kuomba viongozi hao kuombea amani, ametumia fursa hiyo kuwaomba wakichague chama hicho, akisema kina maono ya kuendelea kulinda amani na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari, tofauti na baadhi ya wengine ambao wanahubiri mfarakano.

“Naomba mtuchague CCM. Tukiwa na Rais lakini hatuna wabunge na madiwani, kazi yetu itakuwa ngumu, haitafanyika vizuri. Kwahiyo tunaomba pia mtupigie kampeni, tushinde tukakamishe tuliyoyaanzisha,” amesema.

Dk Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuchagua madiwani kwani wamepanga katika awamu inayokuja kuimarisha zaidi Serikali za mitaa, kwa hiyo itakuwa kazi ngumu iwapo wasipopata madiwani wengi wa kutosha.

Mgombea huyo wa CCM amesema endapo wakipata ridhaa tena, hawana sababu changamoto zilizobakia kwanini wasizimalize. Amesema katika awamu iliyomalizika, wamefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo katika sekta zote, kwa hiyo wanachotaka ni kukamilisha kazi hiyo katika kipindi kinachokuja.

Amesema katika sekta ya elimu wamejenga shule nyingi za ghorofa, zaidi ya vyumba 4,800 vya madarasa, maabara, na kuboresha mishahara ya walimu, na tayari matokeo yameonekana kwani ufaulu umeongezeka.

Katika sekta ya afya, barabara, bandari na maji ni maeneo ambayo amesema yamefanikiwa, lakini wanataka wapewe muda mwingine ili kufanya makubwa zaidi kuendeleza pale walipofikia kwa sasa.

Iwapo chama hicho kikipata ridhaa nyingine, kwa mujibu wa mgombea huyo, wamejipanga kumaliza tatizo la ajira kwa vijana na kushughulikia bei za vyakula, ambazo ndio zinaonekana kuwa matatizo makubwa kwa sasa kisiwani humo.

Kwa upende wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa, amesema kipaumbele kikubwa cha CCM ni amani, kwani inaamini hakuna mbadala wa jambo hilo.

Amesema wakati wanaingia madarakani mwaka 2020 walikutana na viongozi wa dini, na wanapomaliza ngwe hiyo na kuanza nyingine, wameona ni busara kukutana nao ili kuwakabidhi jambo hilo.

“Bila kuwa na amani, mshikamano na umoja, hata ibada zetu hazitafanyika, lakini serikali haitapata fursa ya kuleta maendeleo. Kwahiyo tumeona ni muhimu zaidi kukutana na nyie,” amesema Dk Dimwa.

Kwa mujibu wa Dk Dimwa, viongozi wa dini ndio wenye dhima ya kurudisha umoja na amani katika nchi. Amesema viongozi wa dini ndio wenye watu wengi katika nyumba za ibada, kwahiyo wanasikilizwa zaidi.

Nao baadhi ya viongozi wa dini wamesema kwa sasa nchi ina amani, hivyo ipo haja ya kuiendeleza, ili kupata mafanikio makubwa zaidi.

Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Zanzibar, Askofu Kanani Balinkena, amesema kipindi cha nyuma hata ibada hazifanyiki, “leo watu wanazungumza pamoja, tunaabudu bila tatizo; hili sio jambo la kubeza.”

Amesema ni wajibu wao viongozi wa dini kuendelea kuombea amani, uchaguzi umalize kwa kuwashajihisha waumini wao siku ikifika waende kupiga kura, ambayo ni haki yao kikatiba.

Naye Sheikh Iddi Iddi amesema amani haina mbadala, kwa hiyo lazima waendelee kuiombea nchi isiingie katika mifarakano wakati wa uchaguzi.