MGOMBEA CCM KUIGEUZA BUSERESERE DUBAI YA TANZANIA

::::::::

SIKU moja baada ya kufanyika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025 katika wilaya ya Chato mkoani Geita, mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paschal Lutandula, ameahidi kuubadilisha mji mdogo wa Buseresere kuwa Dubai ya Tanzania iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge.

Kadhalika amemtaka aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chato,Dkt. Medard Kalemani,kulala usingizi mnono kwa madai kuwa ameliacha Jimbo hilo likiwa katika mikono salama na kwamba wananchi wanapaswa kungoja maendeleo kwa kasi kubwa.

Aidha ameahidi kufunga kamera za ulinzi mji mzima ili watu wafanye biashara usiku na mchana kwa lengo kuinua uchumi wa wananchi na kuongeza pato la serikali.

Vilevile amewataka wananchi kumuombea afya njema ili ayatimize matamanio yake, huku akidai akichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo atahakikisha anadhibiti vitendo vya uonevu vinavyofanywa kwa vijana kukamatwa ovyo na badala yake wafurahie matunda mema ya CCM.

Alikuwa kwenye Uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi mkuu katika Jimbo la Chato Kusini zilizofanyika kwenye mji mdogo wa Buseresere wilayani Chato mkoani Geita.

Kwa upande wake, mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Mwl. Cornel Magembe, amesema anayo Imani kubwa kwa wananchi wa wilaya ya Chato kuwa watampigia kura Rais Samia Suluhu Hassan, Wabunge na Madiwani wote kutoka kata 23 za wilaya hiyo.

Hata hivyo amekishukuru CCM kwa umakini mkubwa wa kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya Chama hicho na kwamba wateule wote wanafaa kuchaguliwa kuwa wawakilishi katika maeneo yao.

Awali mmoja wa waliokuwa wa watia nia wa Ubunge ndani ya CCM katika Jimbo la Chato kusini, Mhandisi Deusdedith Katwale, amesema muda uliopo ni kuendelea kujenga nyumba moja kwa kuwapigia kura wagombea wa CCM ili wapate ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Amesema licha ya kwamba hakufanikiwa kuteuliwa na Chama hicho kupeperusha bendera ya Ubunge katika Jimbo hilo, kwa nia ya dhati anaungana na mgombea aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika ngazi ya Ubunge na kwamba kazi ya kuijenga wilaya ya Chato haihitaji kutengana ispokuwa ni kushikamana kwa pamoja kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa haraka.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Chato, Barnabas Nyerembe, amesema katika kutafuta kura za CCM mwaka 2025, chama hicho kimelazimika kuwaalika waliokuwa watia nia ya Ubunge kwenye majimbo ya Chato Kusini na Kaskazini ili kuonyesha umoja na mshikamano uliopo ndani ya Chama hicho.

Aidha amewataka wagombea wa nafasi ya Ubunge kwenye majimbo hayo, kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, maisha mazuri, fedha mfukoni na kwamba kupitia Ilani ya CCM inaelezwa kuwa ndani ya miaka mitano wananchi wawe na maisha bora.

“Nia ya wananchi ni kupata huduma bora za afya, barabara, maji safi na salama, pamoja na kuboreshwa kwa uchumi wa jamii na kwamba wananchi hawawezi kupata maendeleo wanayokusudiwa pasipo kuletwa na CCM” amesema Nyerembe.

Kadhalika amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwaajili ya kuwachagua Rais, Wabunge na Madiwani kupitia Chama hicho.

Jimbo jipya la Chato Kusini,lina kata tisa huku Jimbo la Chato Kaskazini likiwa na kata 14 ambazo zinaifanya wilaya hiyo kuwa na jumla ya Kata 23 huku majimbo yote mawili kukiwa na wagombea wa CCM pekee.