JKT yatinga fainali ya CECEFA

JKT Queens imetinga fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake baada ya kuishinda Kenya Police Bullets kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare ya bao 1-1.

Mechi hiyo imepigwa katika Uwanja wa Moi Kasarani, Naironi Kenya, ambako yanafayika mashindano hayo yaliyoanza Septemba 4 na fainali itapigwa keshokutwa Septemba 16.

JKT sasa itakutana na Rayon Sports ya Rwanda iliyotinga fainali baada ya kuishinda Kampala Queens ya Uganda kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana.

Katika nusu fainali hiyo kila timu ilionyesha nia ya kuitaka mechi na Police ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 14 kwa penalti lililofungwa na Magret Kunihira baada ya kiungo wa JKT, Donisia Minja kumchezea faulo Emily Morang’a.

Baada ya Police kuongoza kwa bao hilo, JKT ilionekana kucheza bila maelewano hasa eneo la kiungo lililokata mawasiliano kutokana na Kunihira kuvuruga safu hiyo akishambulia kwa kasi.

Mechi iliendelea kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini Police ilionekana kutumia nguvu zaidi.

Timu hiyo ilishindwa kukabiliana na hasa mipira ya kushtukiza kwani ikishambulia wanakuwa wazito kurudi chini kukaba hasa pale JKT walipopokonya mipira.  

Dakika 25 za kwanza JKT ilipunguza presha na pasi za kwenda kwa mawinga zilianza kufika hasa upande wa Winifrida Gerald ambaye alionekana kuwa na madhara kwa mabeki wa Police.

Dakika 38, JKT walisawazisha kupitia kwa Jamila Rajabu aliyepiga kwa kichwa akimalizia faulo iliyopigwa na Minja baada ya Winifrida kufanyiwa madhambi na beki wa Police nje kidogo ya 18.

Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika JKT iliushika mchezo ikionekana kushambulia zaidi lango la Police ambao ilikuwa makini kuokoa hatari.

Mabadiliko ya kipindi cha pili yaliyofanywa na kocha wa JKT, Azishi Kondo ya kumtoa mshambuliaji Asha Mwalala na kumuingiza winga Aliya Fikirini yalionekana kuwa na faida kwani awali Mwalala alionekana kuwa mzito hasa kwenye pasi ndefu ambazo alipelekewa.

Hadi mechi inatamatika kila timu ilionyesha upinzani mkubwa na baada ya dakika 90 kumalizika na zile 30 za nyongeza mikwaju ya penati iliamua JKT kwenda fainali ikiwa mara yake ya pili baada ya mwaka 2023 kuchukua ubingwa mbele ya bingwa mtetezi CBE aliyetolewa hatua ya makundi msimu huu.

JKT inakwenda kukutana na Rayon Sports ya Rwanda ambayo ndio mara ya kwanza kucheza fainali ikitinga pia hatua hiyo kwa penalti.

Mshambuliaji kinda wa JKT, Jamila Rajabu amefikisha mabao matano akiwa anaongoza kwenye orodha ya wafungaji, akianza na hat-trick kwenye mechi ya makundi dhidi ya JKU, akafunga bao moja kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Yei Joints na leo akifunga bao la kusawazisha.