RC Malisa apongeza TBS kwa kuwainua wajasiriamali kupitia maonesho ya biashara

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa, ameipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa juhudi zake za kuwafikia na kuwahudumia wajasiriamali kupitia maonesho mbalimbali ya kibiashara nchini.

Akizungumza wakati wa Tamasha la Maonesho ya Kimataifa ya Kusini ya Biashara yanayoendelea mkoani Mbeya, Mh. Malisa alisema hatua ya TBS kutembelea na kutoa msaada wa kitaalamu kwa wajasiriamali ni jambo la kupongezwa na linapaswa kuwa endelevu ili kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Ameeleza kuwa uwepo wa TBS katika maonesho hayo unatoa hamasa kwa wazalishaji wadogo na wa kati kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vya ubora, hatua itakayoongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

RC Malisa pia amewahimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo ushauri wa kitaalamu, ili kuongeza thamani ya bidhaa na kujiwekea msingi thabiti wa kibiashara.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Yekonia Sanga, amesema shirika hilo limehudhuria maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu matakwa ya viwango vya ubora kwa wazalishaji na watumiaji wa bidhaa.

Amesema TBS imewatembelea wajasiriamali katika mabanda yao na wengine kufika katika banda la TBS kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za kupata alama ya ubora pamoja na kushirikisha changamoto zinazowakwamisha katika kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.

Aidha, Mhandisi Sanga amebainisha kuwa Serikali kupitia TBS inatoa huduma ya uthibitishaji wa ubora wa bidhaa bure kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa muda wa miaka mitatu, baada ya kuthibitishwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

“Tunatoa wito kwa wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuongeza wigo wa masoko yao ndani na nje ya nchi. Huduma ya uthibitishaji ni bure kabisa kwa wale watakaotambulishwa kupitia SIDO,” amesisitiza.