Mgombea urais UPDP aahidi viwanda vya kuchakata karafuu akipewa ridhaa

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama Cha UPDP, Hamad Mohamed Ibrahim amesema iwapo wakipata ridhaa ya kuingia madarakani, Serikali ya chama hicho itajikita katika kujenga viwanda kwa ajili ya kusarifi karafuu.

Pia, amesema vijana wataoa bure na mahari zitatolewa na serikali huku mwanamke anayechumbiwa nayeye atapewa Sh1.5 milioni kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

Ametoa kauli hiyo leo Septemba 14, 2025 katika viwanja vya Garagara Mtoni Kidatu wakati wa kuzindua kampeni za chama hicho.

“Serikali ya UPDP itajikita kwenye viwanda, tutajega viwanda vya kusarifu karafuu, tunataka karafuu itakayokuwa inauzwa nje asilimia 80 iwe imeshasarifiwa,” amesema.

Ibrahimu amesema karafuu ni zao muhimu na lenye manufaa makubwa katika uchumi wa mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla.

Katika kuliendea vyema jambo hilo, UPDP inategemea kujenga vinu vya nyukilia ili kukabiliana na changamoto ya umeme ambao utaendesha viwanda na matumizi ya nyumbani

“Lile suala la kukatika umeme, vitu vinaharibika linakwenda kuwa mwisho, tunaomba mtuunge mkono ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu,”

Ibrahimu amesema jambo lingine iwapo vijana wote wenye nia ya kuoa lakini hawana uwezo, watapata fedha kutoka serikalini.

“Anayechumbia atapewa Shilingi milioni mbili na anayechumbiwa atapewa shilingi Sh1.5 milioni ambayo atakwenda kunyia biashara zake na serikali ndio itadhamini harusi,” amesema.

Kwa upande wa wazee, Ibrahimu amesema watawaondolea matatizo ya vijana wao kushindwa kuoa kutokana changamoto ya kukosa kipato.

Akizungumzia wavuvi, mgombea huyo amesema watawekewa mikopo na vifaa vya kisasa wakavue kwa tija ili kuendesha familia zao bila shida yoyote.

Amesema licha ya Serikali iliyopo madarakani kutoa vifaa vya uvuvi, lakini bado hawajafikiwa wote hivyo wakikipa ridhaa chama hicho wanakwenda kumaliza changamoto hiyo.

Naye mgombea wa urais wa chama hicho wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Twalib Kadege amesema wanaohubiri uvunjifu wa amani waondolewe kwenye majukwaa kwani wanachotaka ni maendeleo.

Amesema Serikali ipo mikononi mwa wananchi hivyo watunze kadi zao na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

“Kwahiyo unatakiwa uitunze mpaka tarehe 29 umchague unayemtaka ili akuongoze vizuri kwa kuitambua leo yake na kesho yake, usikubali kukaa nyumbani bila kuona umuhimu,” amesema.

Amesema; “tupo watu wengi inabidi tuchague kwa kishindo kujua Serikali tunayemtaka hata anayeshinda anapata moyo kwamba amechaguliwa vyema.

Amesema wanakusudia kutengeneza serikali wezeshi watanzania waijue kesho yao.

Serikali itatengeneza mazingira mazuri ili wakubaliane na mwekezaji namna watakavyogawana lakini sio Serikali kumiliki ardhi alafu rasimali zilizopo kwenye ardhi hanufaiki nayo.

Amesema hakuna mwekezaji atakayemiliki chochote badala yake watawaachia wananchi ndio wawe wamiliki.

Amesema wakiipa madaraka ndio utakuwa mwisho wa jembe la mkono kwnai wanatarajia kuleta matrekta milioni 400.

Wakulima wakishalima watatafutiwa masoko na kujenga viwanda vikubwa vitakavyowezesha kutoa ajira kwa vijana.