Dar es Salaam. Safari ya mgombea urais wa Chama cha ACT – Wazalendo, Luhaga Mpina kugombea nafasi hiyo imeendelea kukumbana na vikwazo baada ya kuwekewa mapingamizi mengine huku chama hicho kikieleza hatua itakazochukua.
Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo, mapingamizi hayo, yamewekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wagombea urais wa Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) na wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), wakieleza kuwa Mpina hana sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Awali, katika kukabiliana na misukosuko hiyo, ACT – Wazalendo ilifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya mgombea urais wa chama hicho pamoja na kuwasilisha majibu ya mapingamizi waliyowekewa.
“Tulikwenda mahakamani kupinga kauli ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kumuengua mgombea wetu… pia, mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa kauli hiyo hiyo(hajakidhi vigezo) kumuwekea mgombea wetu pingamizi kwa madai utaratibu wa chama haukufuatwa,” amesema Shangwe Ayo, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Septemba 14, 2025.
Kizingiti kwa Mpina kilianzia hapa
Agosti 14 mwaka huu aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT- Wazalendo, Monalisa Ndala alimwandikia barua katibu mkuu wa chama hicho, akipinga uamuzi wa chama kumteua Mpina kuwania urais akidai uteuzi wake ulikiuka kifungu cha 16(1) (4)I cha taratibu za uendeshaji wa chama.
Sakata hilo lilipokewa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ambaye kada huyo alimpatia nakala ya malalamiko yake, hivyo ofisi hiyo kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na katibu huyo mwenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Oktoba 26, 2025, msajili alichukua hatua ya kubatilisha uteuzi wa Mpina kugombea nafasi hiyo kupitia ACT – Wazalendo kwa madai uteuzi haukufuata utaratibu.
Uamuzi huo uliifanya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutopokea fomu ya Mpina, hivyo kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro kwa kutokidhi vigezo vilivyotajwa na ofisi ya msajili.
Hatua hiyo ilimfanya Mpina na ACT-Wazalendo kutinga mahakamani kupinga uamuzi wa kunyimwa fursa ya kurejesha fomu na Septemba 11, 2025 Mahakama Kuu Masjala ya Kuu-Dodoma, ikamrejesha kwenye kinyang’anyiro hicho ikisema kuwa, uamuzi wa INEC kutopokea fomu yake haukuwa sahihi.
Mpina akataa gari la INEC
Baada ya kurejesha fomu na kukabidhiwa gari na INEC, Mpina alikataa jambo ambalo Mwanasheria wa ACT – Wazalendo, Omar Shaaban na mgombea huyo walifafanua kuwa huo ndio msimamo wa chama chao.
Walieleza kuwa gari si kielelezo cha usawa kwenye uchaguzi mkuu, wakati kuna masuala ya sheria, Katiba na kanuni yanayotakiwa kuwekwa katika usawa.
Wakati ACT-Wazalendo wakiwa kwenye furaha ya mgombea wao kurejeshwa,wakiahidi kuanza mchakamchaka wa kampeni, Septemba 12 mwaka huu, mgombea huyo kwa mara nyingine aliwekewa pingamizi.
Akizungumzia sababu ya kumuwekea mgombea huyo pingamizi, mgombea urais wa NRA, Hassan Almas amesema ameweka pingamizi hilo kutokana na mgombea huyo kutokuwa na sifa za kugombea urais.
“Mwenzetu hana sifa ya kuwa mgombea na hakuteuliwa na chama, Mahakama imetoa maelezo na mimi ni mgombea nina haki ya kuweka pingamizi pale ninapoona suala la uchaguzi ni la kisheria,mgombea ana nafasi ya kumuwekea mgombea mwenzake pingamizi Mahakama nayo inaweza kutafsiri,” amesema.
Mwenyekiti wa AAFP, Said Soud Said amesema hafahamu kama kuna pingamizi hilo, bali atafutwe katibu mkuu wa chama hicho atakuwa na ufafanuzi zaidi.
Alipotafutwa Katibu Mkuu, Rashid Rai kuhusu jambo hilo, alisema wapo kwenye mkutano wa hadhara kwa wakati huo atafutwe wakati mwingine.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Msaidizi Uratibu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ipyana Mlilo amesema kisheria, mapingamizi yanaruhusiwa lakini lazima yawasilishwe INEC.
“Mapingamizi yakiwasilishwa tume, pande zote mbili zinapewa fursa, mmoja ataeleza kwa nini kaweka pingamizi na mwingine atatakiwa kujibu na hayo ni mambo ya kawaida na tume itaangalia kama mapingamizi yamekidhi taratibu za kisheria na kutoa uamuzi,” amesema Mlilo.
Mtaalamu wa Sheria, Ado Novemba akizungumzia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka pingamizi kwa mgombea wa ACT – Wazalendo, amesema anasimama kwa niaba ya INEC.
Taarifa ya ACT – Wazalendo
ACT – Wazalendo kupitia taarifa yake kwa umma inaeleza kuwa, wamebaini sura ya mapingamizi hayo ni madai yasiyo na ukweli wala msingi wowote kwamba Mpina hakuteuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama kuwa mgombea urais.
“Katika hati (fomu) ya pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema anamwekea pingamizi mgombea wa ACT – Wazalendo kwa kuwa hana sifa za kuwa mgombea wa kiti cha Rais,” inaeleza taarifa ya ACT- Wazalendo
Pingamizi kutoka kwa mgombea wa NRA, inaeleza mgombea wa ACT – Wazalendo hana sifa za kuwa mgombea wa kiti cha Rais na hakuidhinishwa na chama cha siasa kugombea kiti hicho.
Pia, kwa upande wa mgombea wa AAFP, Mpina hana sifa za kuwa mgombea wa kiti cha Rais/makamu wa Rais na hajakidhi kuidhinishwa na chama cha siasa kugombea.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa umma, ACT – Wazalendo kupitia kwa wanasheria wake wakiongozwa na mwanasheria mkuu wao, Omar Shaaban watajibu mapingamizi yote matatu yaliyowekwa na watayawasilisha ndani ya muda wa kisheria.
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2024, inayozungumzia pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea wa kiti cha Rais na makamu wa Rais, kifungu cha 37 (1) inaeleza kuwa, pingamizi linaweza kuwekwa na mgombea mwingine, msajili wa vyama vya siasa au mwanasheria mkuu wa Serikali, isipokuwa kwa pingamizi chini ya kifungu kidogo cha (1)(e) linaloweza kuwekwa na msajili wa vyama vya siasa pekee; na litawekwa kwa maandishi na kusainiwa na mweka pingamizi na kubainisha sababu za pingamizi.
Kwa mujibu wa kifungu cha (4), tume kabla ya kuamua juu ya uhalali wa pingamizi lolote na bila kuchelewa (a) itamtaarifu mtu aliyewekewa pingamizi; na (b) itampa mtu huyo nafasi ya kusikilizwa.
Kwa mujibu wa kifungu cha (5), endapo tume itatoa uamuzi kuhusu pingamizi lolote chini ya kifungu kidogo cha (3), itamjulisha kwa maandishi mgombea anayehusika kuhusu uamuzi na sababu za uamuzi huo.
Kwa mujibu wa kifungu cha (6), uamuzi wa tume chini ya kifungu hiki utakuwa ni wa mwisho na hautahojiwa na Mahakama yoyote.