Kelvin John aweka chuma mbili Denmark

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Kelvin John anayekipiga Aalborg, amefunga mabao mawili jioni ya leo kufuatia ushindi wa 4-0 dhidi ya Middelfart Boldklub kwenye muendelezo wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Denmark.

Mabao ya John aliyefunga dakika ya 72 na 82, yameisogeza timu hiyo hadi nafasi ya nane kutoka tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo maarufu Danish 1 Division. Kwenye mechi tisa chama hilo limekusanya pointi 11, likishinda tatu, sare mbili na kupoteza nne. 

John ambaye ni msimu wake wa pili kuichezea timu hiyo iliyoshuka Ligi Kuu msimu uliopita, amekuwa na muendelezo mzuri tangu ligi hiyo ianze huku leo akimaliza dakika zote tisini.

Mabao mawili aliyofunga nyota huyo wa zamani wa Genk ya Ubelgiji, yanamfanya kufikisha jumla ya mabao matano kwenye mechi tisa alizocheza akiwa kwenye tatu bora ya wafungaji wa ligi hiyo, huku anayeongoza Andersen Kasper akiwa nayo saba.

Kiwango alichoonyesha kwenye mechi tisa za ligi zimemfanya kukubalika na mashabiki jambo ambalo limemfanya kunyakua tuzo mbili za nyota wa mechi ‘Man of the Match’ na utaratibu wa kumpata mshindi anapigiwa kura na mashabiki kupitia APP na atakayepata kura nyingi anaondoka na tuzo hiyo.

Hilo linathibitisha namna gani John anakubalika kwenye kikosi hicho kwani anapofunga bao mashabiki wanamshangilia wakitaja jina la nyota huyo wa Kitanzania.

Katika ushindi huo, mabao mengine ya Aalborg, yametokana na kiungo wa Middelfart Boldklub, Mathias Greve kujifunga dakika ya 49, kisha Valdemar Møller akahitimisha kwa bao la dakika ya 90+3.

Mbali na John, Watanzania wengine wanaocheza mataifa mbalimbali nje ya Afrika, wikiendi hii walikuwa na kibarua cha kuzipambania timu zao akiwemo Alphonce Mabula anayeitumikia Shamakhi FC ya Ligi Kuu Azerbaijan, alifunga bao moja kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Karvan, Enekia Lunyamila wa FC Juarez ya Wanawake nchini Mexico aliifungia bao timu hiyo ikiondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cruz Azul huku Mbwana Samatta (Le Havre) akimaliza dakika 90 chama lake likipoteza 1-0 dhidi ya Strasbourg kwenye muendelezo wa Ligi Kuu Ufaransa.