Kingu asaka kura za wagombea wa CCM Jimbo la Songea mjini

Songea. Aliyekuwa mbunge wa Singida Magharibi, Elibarik Kingu amewataka wananchi wa Jimbo la Songea kutofanya kosa bali waendelee kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema kimetekeleza kwa vitendo ahadi zake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 14, 2025 kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika viwanja vya Kiblang’oma, Kata ya Lizaboni, Kingu amesema chama hicho kimefanikisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uhasibu kinachoendelea kujengwa eneo la Mlete, kuboresha huduma za afya, maji, miundombinu ya barabara, pamoja na kutoa ruzuku ya mbolea kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo ili kumwezesha mkulima kuepuka gharama kubwa za pembejeo.

Kingu ametumia nafasi hiyo kunadi Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030, akieleza kuwa katika kipindi kilichopita, Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanikisha ujenzi wa vituo vya afya vinane, Hospitali ya Rufaa, vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari, uboreshaji wa barabara kwa kiwango cha lami, vivuko, madaraja na mradi mkubwa wa maji wa miji 28 wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 147.

Katika mkutano huo, wagombea wa nafasi za udiwani kutoka kata 21 pamoja na madiwani wa viti maalum walijinadi na kuwaomba wananchi kura sambamba na kumuombea kura mgombea wao wa urais, Samia Suluhu Hassan na mgombea ubunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro.

Kwa upande wake, Dk Ndumbaro amesema kuwa katika kampeni za mwaka 2020, CCM iliwaahidi wananchi ruzuku ya mbolea, kutafuta soko la mazao, kuboresha huduma za afya, elimu, maji, pamoja na uboreshaji wa uwanja wa ndege.

Alitaja pia malipo ya fidia katika Bonde la Mto Ruhila yenye thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni pamoja na uwekaji wa taa za barabarani.

“Rais Samia pia amewaletea msaada wa kisheria kupitia Mama Samia Legal Aid. Katika Ilani mpya, CCM imeahidi kuendeleza ruzuku ya mbolea kwa miaka mitano ijayo na kutekeleza miradi mingine mikubwa ya maendeleo,” amesema Dk Ndumbaro.

Amesema kutoka na ahadi zote walizoziahidi kutekelezwa, ni wakati mwafaka kwa wananchi kukirudisha madarakani chama hicho kwa kutoa kura zote za ndio kwa wagombea wake wote kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na rais ikifika Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi mkuu.