Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema endapo akishika madaraka Oktoba 29, mwaka huu atahakikisha anajenga demokrasia ili Wazanzibari wawe huru kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi huru.
Amefafanua kuwa Serikali atakayoiunda itakomesha utaratibu wa viongozi kuchaguliwa kwa njia zisizo halali, hali inayosababisha Wazanzibari kupokwa haki yao ya kuchagua wanayemtaka kupitia sanduku la kura.
Ameeleza hayo leo Jumapili, Septemba 14, 2025, wakati akizindua kampeni zake kwa upande wa Unguja katika uwanja wa Kibanda Maiti, baada ya jana Jumamosi kuzindua kisiwani Pemba katika uwanja wa Tibirinzi wilayani Chakechake.
Amesema wanakwenda kuitengeneza Zanzibar iliyo bora na kuirejesha mikononi mwa Wazanzibari kwa kuweka utaratibu wa haki ya kupiga kura katika chaguzi huru na haki.

Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, amesisitiza kuwa katika utawala wake ataliondoa suala hilo ili kuleta haki kwa wananchi wa visiwa hivyo.
Othman amejenga hoja kupitia kipaumbele chake cha kwanza cha Katiba mpya, ambayo itapatikana endapo akifanikiwa kushika dola, ili kuweka mazingira ya usawa na utawala wa sheria kwa Wazanzibari.
“Katiba mpya ndicho kipaumbele chetu cha kwanza na Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar mtakayoichagua kwa mapendekezo yenu,” amesema Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa, amesema hoja tatu ikiwemo uzalendo na uaminifu ndizo zinazombeba mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Othman.
Hoja nyingine ni uwajibikaji na kiongozi anayejali maisha ya Wazanzibari, akitaka waishi vizuri.
“Uchaguzi huu utaamuliwa na hoja tatu zitakazowaongoza wapigakura wa Zanzibar wakifika kwenye sanduku la kura. Nataka mkifika kwenye sanduku la kura mjiulize nani anafaa kuwa Rais kupitia hoja hizi tatu, ikiwemo ya Othman kuwa mtu mzalendo, mtii na mwaminifu kwa Wazanzibari. Huyu si mwingine, ni Othman ambaye hatafuni maneno katika kusimamia maslahi na haki za Wazanzibari,” amesema Jussa na kuongeza:
“Ndani ya miaka mitano, kwa nyakati tofauti, Othman amekuwa akikemea ufisadi na akitaka wachukuliwe hatua. Huu ndiyo uwajibikaji, hili si la ACT Wazalendo, la watu wote maana dhiki inatukumba wote.”
Jussa amesema mgombea urais wa chama hicho, Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, ni chaguo la uwajibikaji na atakayeiletea heshima Zanzibar.
“Uchaguzi huu ni chaguo la maisha mazuri kwa Wazanzibari, si kikundi cha watu. Tunakwenda kuueleza maana ya uchaguzi huu kwa kiongozi anayepigania maisha ya Wazanzibari, si kikundi cha watu wachache. Miaka mitano hii, kila mtu alikuwa analalamika, si mkulima, mfanyabiashara wala bodaboda, kila mwananchi analalamika njaa, ajira na maisha magumu,” amesema Jussa.
Othman atainua uchumi Zanzibar
Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Juma Duni Haji ‘Babu Duni’, amesema mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ndiye kiongozi sahihi atakayeleta mabadiliko ya kuinua uchumi wa Wazanzibari.

Amefafanua kuwa, kwa mazingira ya sasa, Zanzibar inahitaji mabadiliko yatakayowezesha wananchi wa visiwa hivyo kumudu milo mitatu kwa siku.
“Kinachohitajika kwa sasa ni mabadiliko yaliyosubiriwa kwa muda mrefu. Mtaani kuna ugumu wa maisha, kila mtu analalamika njaa… Tuamue tukampigie kura zote Othman Masoud, ndiye atakayetutoa hapa tulipo,” amesema Babu Duni, ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa ACT Wazalendo.