MASHABIKI wa soka hususan wale wa Simba na Yanga kwa sasa wanahesabu saa tu kabla ya kuzishuhudia timu hizo zikishuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuvaana katika mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-2026.
Zimesalia saa 24 tu kabla ya vigogo hivyo kukutana kwa mara ya kwanza msimu huu katika mechi inayoonekana ni mtego kwa timu zote itakayopigwa kuanzia saa 11:00 jioni, huku kila moja ikiwa imetoka kutesti mitambo katika matamasha ya Simba Day na Kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Mechi hiyo itapigwa kesho Jumanne, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana siku hiyo kwa Ngao ya Jamii, ila itakuwa ni ya tatu kwa watani hao kukutana, huku namba zikiibeba Simba zaidi kuliko Yanga ambao ndio watetezi wa taji hilo sambamba na Ligi Kuu na Kombe la FA.
Ndiyo, rekodi zinaonyesha klabu hizo zimeshakutana mara mbili katika mechi za Ligi ya Bara tangu mwaka 1965, huku Yanga ikipasuka zote ikiwamo kile kipigo kinene cha mabao 6-0 kilichopatikana Julai 19, 1977 na kushuhudiwa hat trick ya kwanza na ya pekee katika Dabi ya Kariakoo.
Mechi hiyo ilipigwa Jumanne na mshambuliaji, Abdallah ‘King’ Kibadeni alifunga mara tatu katika dakika ya 10, 42 na 89 na kuifanya rekodi yake ya hat trick kushindwa kuvunjwa kwa miaka 48 sasa kama ambavyo Yanga inavyosota kulipa kisasi hicho cha kupigwa mabao 6-0 na watani wao hao.
Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na beki wa Yanga, Selemani Sanga aliyejifunga alipokuwa akipambana kuokoa mpira dakika ya 20 na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ alitupia mara mbili dakika ya 60 na 73 na kuifanya Simba kulipa kisasi cha kupigwa 5-0 na Yanga Juni 1, 1968.
Mechi nyingine iliyopigwa Jumanne, ilikuwa ni ile ya Oktoba 27, 1992 na Simba iliibuka wababe kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Damian Kimti, kikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Wanajangwani kwa msimu huo, kwani ilipoteza pia mechi ya kwanza 2-0 iliyopigwa Septemba 26.
Hivyo, kesho itakuwa ni mechi ya mtego kwa Yanga kutaka kujikomboa katika unyonge wa kupigwa kila inapokutana na Wekundu wa Msimbazi siku hiyo ya Jumanne na iwapo itapoteza tena wababe hao wataendelea kuwa wanyonge kwa watani wao kila inapokutana nao katika siku hiyo.
Kwa upande wa Simba itakuwa ni mtego wa kutaka kuendeleza ubabe wa siku hiyo ya Jumanne, lakini ikiwa na deni la kufungwa mechi tano mfululizo zilizopita za mashindano na watani wao hao. Ndiyo, Simba haijaonja ushindi mbele ya Yanga tangu iliposhinda 2-0 katika mechi ya marudiano ya Ligi ya msimu wa 2022-2023 iliyopigwa Aprili 16, 2023 kwa mabao ya Henock Inonga na Kibu Denis, kwani baada ya hapo imekumbana na vipigo ikiwamo ile ya 5-1 ya Novemba 5, 2023.
Mechi nyingine Simba ilizochezea vichapo ni ile ya Aprili 20, 2024 iliponyukwa 2-1, kisha ikapasuka katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya msimu uliopita kwa bao 1-0 la Maxi Nzengeli, kabla ya kucharazwa nje ndani katika Ligi Kuu msimu uliopita ikianza na kipigo cha 1-0 kisha 2-0 kilichowapa Yanga ubingwa wa 31 tangu 1965 na wa nne mfululizo tangu walipoipoka Simba.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha hakuna mbabe baina ya timu hizo katika mechi za Ngao ya Jamii kwani zimekutana mara 10 na kila moja kushinda mara tano, licha ya kwamba kwa jumla wa michuano hiyo tangu 2001, Wekundu wa Msimbazi ndio wababe wa kubeba mara nyingi.
Simba imetwaa Ngao ya Jamii mara 10, kuanzia mwaka 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019, 2020 na 2023, huku Yanga ikifuatia nyuma yao ikitwaa mara nane katika miaka ya 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022 na 2024.
Azam na Mtibwa Sugar zinafuata zikitwaa mara moja kila moja, Wanalambalamba ilibeba 2016 na Wanatamutamu walitwaa 2009 zote zikiifunga Yanga.
Kwa jinsi vikosi vya timu hizo zilivyo kwa sasa na aina ya makocha, ni wazi kesho kutakuwa na kazi kubwa ya kuamua mbabe wa Ngao, kwani lolote linaweza kutokea licha ya rekodi hizo za hapo juu.