FAINALI ya michuano ya Kombe la Cecafa Kagame itapigwa leo Jumatatu na Singida Black Stars itavaana na Al Hilal Omdurman ya Sudan kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar es Salaam mara baada ya mechi ya mshindi wa tatu kati ya APR ya Rwanda na KMC inayopigwa saa 6:00 mchana.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Singida BS na Al Hilal kucheza fainali ya michuano hiyo mikongwe zaidi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyoasisiwa mwaka 1967.
Hadi kufika hatua hii, Singida imeshinda mechi tatu kati ya nne, zikiwamo mbili za makundi dhidi ya Polisi Kenya (2-1) na Garde-Cotes ya Djibout (1-0) na moja nusu fainali ambayo ilipigwa juzi, Jumamosi dhidi ya vijana wa Kinondoni, KMC (2-0).
Huku ikitoa suluhu moja katika mechi yake ya kwanza kabisa ya michuano hiyo ya 47 dhidi ya Coffee ya Ethiopia, hivyo chama hilo linalonolewa na Miguel Gamondi lina wastani wa ushindi kwa asilimia 75, ikiwa na wastani wa kufunga bao moja (1.25) kwenye kila mechi.
Singida imeruhusu bao moja tu katika michuano hiyo tofauti na Al Hilal iliyoruhusu manne, hivyo kuwa na wastani wa kuruhusu bao kila mechi.
Al Hilal imeinga fainali baada ya kuichapa APR ya Rwanda juzi kwenye nusu fainali iliyopigwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1 na mwishowe kushinda 3-1, miamba hiyo ilivuka makundi ikiwa kinara wa Kundi C ikikusanya pointi tano kwa kushinda mechi moja dhidi ya Kator kwa mabao 3-1.
Pia ilitoka sare mbili dhidi ya Madani (1-1) na Mogadishu (1-1).
Kwa matokeo hayo katika mechi nne zilizopita hadi kufika fainali, Al Hilal ina wastani wa ushindi kwa asilimia 50, ikizidiwa asilimia 25 na Singida BS.
Tofauti na Singida BS yenye mabao matano ya kufunga, Al Hilal inaonekana kuwa bora zaidi eneo hilo, imefunga mabao manane, hivyo ina wastani wa kufunga mawili kwa kila mechi moja.
Miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuwa na ushindani mkali katika mechi ya leo ni eneo la kati ambalo kwa Singida limeimarika hasa baada ya ujio wa Khalid Aucho aliyekuwa katika jukumu la timu ya taifa ya Uganda akisajiliwa kutoka Yanga aliyoitumikia kwa misimu minne mfululizo.
Aucho alikuwa na muunganiko mzuri na Clatous Chama aliyefunga bao la kwanza katika mechi ya nusu fainali dhidi ya KMC, huku kwa Al Hilal eneo hilo lina Abdelrazig Omer aliyejiunga na kikosi hicho ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya timu ya taifa la Sudan.
Katika mechi ya nusu fainali, Omer alifunga chuma moja wakati Al Hilal ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya APR.
Gamondi alisema kikosi hicho kipo katika hali nzuri kwa mechi hiyo ya fainali; “Natarajia itakuwa mechi nzuri. Kila wakati nalenga kushinda na naamini kesho (leo) pia tutashinda. Lengo letu si tu kushinda Kagame Cup, bali pia kujiandaa kwa msimu mrefu tulio nao mbele michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu NBC. Lakini hatua ya kwanza ni kushinda na kuchukua ubingwa.”
Kocha huyo hakusita pia kuwatumia salamu mashabiki wa Singida, akiwataka waendelee kuungana na timu hiyo.
“Mashabiki lazima waendelee kuwa nyuma ya kikosi. Tumejitolea kufanya kazi kwa bidii na kuonyesha soka safi linaloiwakilisha Singida na mkoa mzima. Tunataka kupigania nafasi nne bora kwenye ligi na kwenda mbali kwenye Kombe la Shirikisho,” alisema.
Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia kombe na zawadi ya Dola 30,000 (kama Sh 75 milioni) pamoja na medali za dhahabu, wakati mshindi wa pili atapata Dola 20,000 (zaidi ya Sh50 milioni) na medali za fedha, huku ya tatu itaambulia Dola 10,000 (zaidi ya Sh24milioni) na medali za shaba.