Mtanzania aanza na Al Ahly

JANA Chama la Mtanzania, Arafat Masoud ‘Konde Boy’ anayekipiga ENPPI lilikuwa kibaruani kwenye muendelezo wa Ligi Kuu Misri dhidi ya Al Ahly na nyota huyo alitarajiwa kuwepo kikosini kwa mara ya kwanza tangu alipotambulishwa hivi karibuni.

Kinda huyo alijiunga na timu hiyo akitokea Azam FC aliyoitumikia kwa misimu minane tangu ajiunge mwaka 2017 akicheza timu za vijana za U-17 na U-20 kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa na msimu uliopita aliichezea Fountain Gate kwa mkopo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Konde Boy alisema kulikuwa na changamoto na baadhi ya mambo hayakukamilika hivyo mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu huenda ikawa dhidi ya Al Ahly.

Aliongeza, kusingekuwa na changamoto ya mambo ya usajili basi tayari angecheza mechi nne za Ligi Kuu kwani kocha alimuweka kwenye mpango lakini ilishindikana kutokana na taratibu hazikukamilika.

“Kwa sasa mambo yako sawa, Pre Season nilicheza lakini hapa kati kulikuwa na mambo hayajakamilika ndiyo maana sikuonekana kabisa uwanjani,” alisema Konde Boy na kuongeza;

“Siku 21 nilizokaa Misri nimeanza kuzoea mazingira ya huku kuanzia hali ya hewa ni joto kali sana, hainipi shida kwa sababu nimeizoea nyumban, vyakula pia sio shida kwa sababu Azam pia tulikuwa tunakula aina hiyo.”

“Labda changamoto kubwa kuzoeana na watu na lugha yao ni Kiarabu na wengine Kifaransa ndio kidogo shida lakini naelewana nao hivyo hivyo vingine kawaida.”

ENPPI iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Misri kwenye mechi tano, ikishinda mbili, sare mbili na kupoteza moja ikiwa na pointi nane sawa na chama la nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, Pyramid FC likiwa nafasi ya saba.