ALIYEKUWA beki timu ya vijana ya Simba, Alon Okechi Nyembe amesajiliwa na Zanaco inayoshiriki Ligi Kuu Zambia kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Beki huyo alicheza Simba U-20 misimu miwili kisha kupandishwa timu kubwa, ingawa aliishia benchi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nyembe alisema kusajiliwa na Zanaco ni fursa kwake ya kuonyesha uwezo wake baada ya kuaminiwa na kikosi hicho.
Aliongeza ni mara yake ya kwanza kusajiliwa na timu kutoka nje ya Tanzania na matarajio yake ni kufanya vizuri na atapata uzoefu kwenye ligi hiyo.
“Nimesaini mkataba juzi wa mwaka mmoja, sina mengi ya kuzungumza lakini naamini nikipata nafasi ya kucheza itaniongezea kitu,” alisema beki huyo mwenye uwezo wa kucheza kati na pembeni.
Wakala wa mchezaji huyo, Hon Simbeye ambaye ni mzaliwa wa Zambia aliliambia Mwanaspoti mchakato wa kumpata beki huyo ulionekana kwenye mechi ya kirafiki.
“Nilimwona kwenye mechi ya kirafiki nikaomba mawasiliano yake. Wakati huo Zanaco waliniambia wanahitaji beki wa kati, kwa hiyo nilipomwona nikampeleka, akaenda kuangaliwa siku tatu Zambia na wakamkubali na kusema anatufaa,” alisema na kuongeza;
“Nimefanya kazi kwa muda hasa na klabu za Ligi Kuu Zambia, kwa aina ya uchezaji wa Nyembe naamini anaweza kuwa na manufaa kwa Zanaco, kwanza ana nidhamu kubwa, isitoshe bado mdogo.”
Kwenye ligi ya Zambia, Zanaco imekuwa na historia ikinyakua mataji saba ya Ligi Kuu na makombe mengine kama Zambian Cup mara moja mwaka 2002, ABSA Cup (2017), Zambian Charity Shield mara nne (2001, 2003, 2006, 2019), Zambian Challenge mara tatu (1987, 1988, 2006) na mengine.
Kimataifa iliwahi kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 2020 ikichapwa mabao 3-1 na Pyramids ya Misri na ilifika hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi C ikiwa na timu kama RS Berkane, DC Motema Pembe ya Congo na ESAE iliyomaliza mkiani mwa kundi hilo.
Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika haina rekodi nzuri kwani imeshiriki mara saba lakini ilicheza makundi mara moja mwaka 2017 zingine iliishia raundi ya pili.