Simbu aiandika rekodi Duniani akiipa Tanzania dhahabu ya kwanza

Historia imeandikwa kwenye mashindano ya Dunia ya Riadha 2025 baada ya mwanariadha, Alphonce Simbu kuibuka kinara wa mbio hizo na kuipa Tanzania medali ya dhahabu ya kwanza kwenye mashindano hayo yaliyofanyika asubuhi ya leo Septemba 15, 2025 Jijini Tokyo, Japan.

Simbu ameandika historia hiyo baada ya kumaliza mbio za kilomita 42 kwa saa 2:09.48 huku akipata upinzani mkali kutoka kwa Amanal Petros wa Ujerumani ambaye pia alikimbia muda sawa (2:09.48) na kushika nafasi ya pili, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Iliass Aouani wa Italia.


Mwanariadha huyo licha ya kumaliza muda mmoja na Petros ushindi wake umeamuliwa na teknolojia baada ya mguu wake kuwa wa kwanza kugusa ardhi baada ya kuvuka mstari wa mwisho.

Ushindi huo unamfanya Simbu kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama Mtanzania wa kwanza kushinda taji la Dunia katika riadha.