Mbeya. Mgombea ubunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Patrick Mwalunenge ametaja miongoni mwa vipaumbele vyake kuwa ni kuboresha miundombinu ya masoko, kujenga kumbi za kisasa za mikutano na hoteli ya nyota tano ili kubadilisha taswira ya jiji hilo.
Amesema atatenga maeneo ya ujenzi wa vibanda vya wajasiriamali wanaopanga bidhaa chini pamoja na kuanzisha jengo maalumu la kunyonyeshea watoto ili kuwasaidia akina mama wanaojihusisha na biashara.
Mwalunenge amebainisha hayo leo Jumapili Septemba 14, 2025 katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Kituo cha Mabasi Kabwe, akiahidi pia kushughulika na vitendo vya uzembe na manyanyaso kwa wagonjwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa afya.
Aidha, amesema atahakikisha anasimamia utekelezaji wa agizo la mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, la kupiga marufuku hospitali za Serikali kuzuia miili ya marehemu kwa sababu ya madeni.
Katika mkutano huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ amewataka wagombea wa ubunge mkoani Mbeya kumnadi Samia ili kupata kura nyingi, huku akisisitiza kuanza mara moja kushughulikia kero za vijana wa bodaboda na bajaji wanaodaiwa kuteswa na askari polisi na migambo.
Naye Mjumbe wa NEC Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela smewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa “mafiga matatu” yaani Rais, Mbunge na Diwani kupitia CCM.
Kwa upande wao, baadhi ya waendesha bodaboda akiwemo Jorace John wameunga mkono wito wa viongozi hao, wakidai uonevu wanaofanyiwa unawaathiri na kuichafua taswira ya Serikali.