Mwanza. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii katika Jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, endapo kitapewa ridhaa ya kuunda serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Jumapili, Septemba 14, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, mgombea urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amesema serikali yake itatoa miezi 18 kwa wawekezaji waliobinafsishiwa viwanda vya mazao ya kimkakati ikiwemo kiwanda cha nguo cha Mwatex kuvifufua na kuviendesha, la sivyo vitarejeshwa serikalini.
“Wakishindwa, navirejesha serikalini. Serikali nitakayoiongoza itawekeza fedha, itatengeneza ajira kwa vijana na kuondoa umaskini,” amesema huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akitolea mfano wa viwanda vya pamba vilivyoko Mwanza, Mwalimu amesema vimenunuliwa na wawekezaji kutoka mataifa makubwa lakini havijaendelezwa, bali vimeachwa vife ili kuendeleza maslahi ya viwanda vyao vya nje.
Upimaji wa ardhi na mikakati ya maendeleo
Katika hatua nyingine, Mwalimu ameahidi kupima ardhi yote ya Jiji la Mwanza ili kuwawezesha wananchi kutumia ardhi kama dhamana ya mikopo au kuwekeza, badala ya kuendelea kuishi katika makazi yasiyo rasmi.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupambana na umaskini kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya wananchi.
SGR, Kilimo na uzalishaji viwandani
Akigusia miundombinu na sekta ya kilimo, Mwalimu ameahidi kusimamia kikamilifu ujenzi na ukamilishaji wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Makutupora hadi Mwanza, akiitaja kama mhimili wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.
“Ndani ya miaka mitano, nitahakikisha asilimia 10 ya bajeti ya taifa inaelekezwa kwenye kilimo. Tutakiunganisha kilimo na viwanda vikubwa na vya kati. Nitarejesha hadhi ya zao la pamba,” amesema.
Amesema serikali yake itafungua viwanda vinavyoendana na mazao ya kimkakati, kuboresha mazingira ya sekta binafsi, na kusambaza maji safi kwa wakazi wote wa Mwanza.
Rasilimali za Taifa na Mapungufu ya uongozi
Mwalimu pia ameikosoa serikali iliyopo madarakani kwa kushindwa kutumia utajiri wa rasilimali za taifa kama madini, ardhi, na maji kwa faida ya wananchi.
“Tanzania ina kila kitu: madini, mito, bahari, ardhi yenye rutuba, na watu wema. Lakini changamoto kubwa ni uongozi mbovu unaosababisha mgogoro kati ya watawala na wananchi,” amesema.
Amesisitiza kuwa taifa lina uwezo wa kujikwamua kiuchumi iwapo litaongozwa kwa fikra sahihi, akiahidi kuwa ndani ya miaka mitano ataondoa umaskini unaoitesa nchi.
Uvuvi, maji na mahitaji ya msingi
Katika mkutano wa awali uliofanyika Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela, Mwalimu alieleza kuwa Chaumma kitarejesha heshima ya sekta ya uvuvi kwa kutoa vifaa na teknolojia ya kisasa kwa wavuvi wa Ziwa Victoria.
“Haiwezekani tuna ziwa lakini hatunufaiki nalo. Chaumma italeta mabadiliko ya kweli,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali yake itahakikisha wananchi wanaopakana na Ziwa Victoria wanapata maji safi na salama, jambo alilosema haliwezekani kuendelea kupuuzwa.
Ahadi kwa Wananchi na wito wa mabadiliko
Akiwaomba kura wakazi wa Jiji hilo, Mwalimu amesema: “Popote mtakaponituma, nitakwenda. Nitumeni nikawatumikie. Sioni sehemu ambayo siwezi kutumika kama kweli nia ni kuwatumikia Watanzania.”
Kwa upande wake, Veronica Mgeta, mgombea ubunge wa Ilemela kupitia Chaumma, amesema wananchi wa jimbo hilo wamekosa mwakilishi wa kweli kwa zaidi ya muongo mmoja. Aliahidi kuleta mtambo wa kukaushia dagaa ili kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, pamoja na kushughulikia matatizo ya maji, umeme na barabara.
“Tunaishi kwa mateso ilhali tupo karibu kabisa na Ziwa Victoria. Hili haliwezi kuvumilika tena,” amesema.