Bado Watatu – 29 | Mwanaspoti

BAADA ya kunipakia kwenye pikipiki nilimwambia: “Mdogo wangu, usipende kujitia katika mambo yasiyokuhusu. Hata kama hiyo namba ya gari umeiona, usiiseme — unaweza kuja kupata matatizo.”
“Kaka yangu amenionya sana. Achilia mbali namba, hata kueleza kuwa nimeliona hilo gari nimekoma.”
“Wakati mwingine polisi wanaweza kukurubuni ili uwatajie.”
“Hao polisi watanijuaje?”
“Huyo msichana aliyekupigia simu anaonekana ana kidomodomo sana.”
“Nitamkana mchana kweupe. Mimi sitaki matatizo.”
Tulipofika barabara ya ishirini nikamwambia kijana huyo asimamishe pikipiki.
“Mimi naona sitakwenda tena Mikanjuni hii leo. Nitakwenda kesho,” nikamwambia kisha nikamlipa pesa zake.
Nilirudi nyumbani kwa miguu. Ile safari ya Mikanjuni ilikuwa ni geresha tu. Nilipomwambia Mudi anipeleke Mikanjuni kwenye msiba nilitaka aone nilikuwa na sababu ya kumdadisi kuhusu Shefa. Na pia nilitaka aone nilikuwa na sababu ya kumfuata pale kituoni kwake. Vinginevyo, kama ningezungumza naye kisha nikaondoka, ningemtia wasiwasi.
Wakati natembea haraka kurudi nyumbani, kidogo niliona moyo wangu umetulia. Ulitulia kwa sababu nilipata uhakika kutoka kwa Mudi kwamba hatapenda kujihusisha na lile tukio.
Kama kweli Mudi aliziona namba za gari langu au hakuziona, kwa vile amesema hatazitaja kwa sababu hakutaka kujitia katika ushahidi wa tukio hilo, lilikuwa ni jambo jema kwangu.
Nafika nyumbani niliona jambo lililonigutusha. Niliona polisi watatu pamoja na mtu mmoja aliyevalia kiraia wakilikagua lile gari la Shefa. Gari la polisi lilikuwa limesimama upande wa pili wa barabara.
Nilifungua mlango nikaingia ndani na kutoa kichwa nje ya mlango kuwachungulia polisi hao.
Sikuweza kujua nini kilikuwa kimetokea. Nikajiuliza iwapo gari la Shefa limegunduliwa au mwenye ile nyumba alitoa taarifa polisi baada ya kuona lile gari limekaa mbele ya nyumba yake kwa siku kadhaa bila mwenyewe kujitokeza.
Kitendo kile cha kuwaona wale polisi kikaanza kunitia hofu upya. Funguo ya gari hilo nilikuwa ninayo mimi. Shefa alipoliacha gari hilo alikuja kwangu; mlinzi alimuona. Lakini kwa wakati ule sikumuona yule mlinzi.
Niliendelea kusimama hapo kwenye mlango nikichungulia. Baada ya muda kidogo nikaona gari lenye kifaa cha kukokota magari likiwasili. Bila shaka polisi hao walikuwa hapo wamefika muda mrefu.
Gari la Shefa likafungwa mnyororo upande wa mbele, likakokotwa na kuondolewa mahali pale. Polisi hao pamoja na yule mtu mwingine wakajipakia kwenye gari la polisi lililokuwa upande wa pili wa barabara na kuondoka.
Ndipo nikafunga mlango na kwenda chumbani kwangu. Nilifika kukaa kitandani na kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nilijiuliza: polisi wameligundaje gari hilo? Je, ni mwenye ile nyumba aliyewapa taarifa au waliligundua wenyewe?
Pia nilijiuliza: polisi hao wamegundua kwamba gari hilo ni la Shefa aliyeuawa na kutupwa makaburini, au wameona ni gari lililotelekezwa na mwenyewe alikuwa hajulikani; na kwa hivyo wameliondoa kwa usalama zaidi?
Nikaendelea kujiuliza, kama polisi wamegundua kuwa ni gari la Shefa na ndiyo sababu waliliondoa, je, nini kitatokea?
Nilijaribu kukisia tu kwamba polisi watashuku kwamba Shefa alifika na gari hilo mahali pale kabla ya kuuawa. Kwa vile hakulichukua tena gari lake, polisi watahisi kwamba Shefa aliuawa katika mtaa huo niliokuwa ninaishi.
Kitu ambacho watakifanya polisi, niliendelea kukisia, ni kutafuta Shefa alipoliacha gari lake alikwenda wapi. Wakigundua alipokwenda au nyumba aliyoingia watajua kuwa Shefa aliuawa ndani ya nyumba hiyo.
Jinsi nilivyokuwa ninawajua polisi, lilikuwa jambo dogo tu kugundua Shefa alikwenda wapi baada ya kuacha gari lake mahali pale. Kwa vile mlinzi wa ile nyumba alimuona Shefa usiku ule, anaweza kuwaambia polisi kuwa mwenye gari hilo aliingia nyumbani kwangu saa sita usiku na hakumuona kutoka tena.
Polisi wakija kupata ushahidi mwingine wa Raisa kwamba waliona mwanamke aliyekuwa akiendesha gari langu ambaye aliutupa mwili wa Shefa kwenye makaburi, ndio nimekwisha!
Mbio zangu za sakafuni zitakuwa zimeishia ukingoni!
Hapo hapo niliona mwili wangu ukifumka joto. Sikujua kama ni presha yangu ilikuja juu au ilikuwa hofu, lakini nikajihisi nilikuwa katika wakati mgumu sana.
Kama si kiherehere changu cha kukubali ushawishi wa Raisa, yasingenitokea haya, nikajiambia.
Jamani mume wa mtu sumu! Tena sumu kali kuliko ya nyoka! Nilijaribu siku moja tu nimeangazika! Nilitafuta pa kuiweka roho yangu, sikupaona!
Kulikuwa na kila dalili kwamba hatima yangu ilikuwa kukamatwa na kushitakiwa kwa mauaji. Wakati wa kuwaeleza ukweli polisi kwamba Shefa aliuawa na mwizi aliyekuja usiku nyumbani kwangu, ulikuwa umeshapita!
Nikaanza tena kulia. Nililia kwa kujua kuwa hatima yangu itakuwa ni kunyongwa tu. Mazingira yaliyotokea kwa Shefa kuuawa nyumbani kwangu usiku na mimi kukaa na mwili wake kwa siku mbili kisha nikaonekana ninautupa katika maeneo ya makaburi saa sita usiku yanaonyesha kuwa mimi ndiye niliyemuua Shefa.
Hapo nisingekuwa na utetezi wowote hata niwe na mawakili arobaini.
Simu yangu iliita; nikagutuka na kuitazama. Nikaona namba ya Suzana. Nikaacha kulia na kujifuta machozi kisha nikaipokea.
“Suzana za huko?” nikauliza nikiifanya sauti yangu kuwa ya kawaida ili asigundue kuwa nilikuwa ninalia.
“Nzuri. Uko wapi?”
“Niko nyumbani.”
“Hutarudi tena huku?”
“Sitarudi. Muda wako ukifika funga tu, tutaonana kesho.”
“Sawa.”
Suzana akakata simu.
Sasa yakanijia mawazo kwamba kesho asubuhi niondoke pale nyumbani, niende nikashinde Sahare kwa wazazi wangu. Kama itabidi niwaeleze ukweli wangu nitawaeleza ili kama nitakamatwa wajue tatizo lililokuwa limetokea.
Usiku ule nililala bila kula kitu chochote. Yapata saa saba usiku nikaamshwa na mlio wa simu. Mume wangu alikuwa ananipigia. Nikapokea simu yake na kumuuliza: “Habari za huko?”
“Nzuri,” akanijibu, lakini sauti yake ilisikika kwa mbali. Akaongeza, “Nimefika Dar sasa hivi. Kesho naweza kuwa huko.”
“Vipi kuumwa?”
“Hali yangu bado si nzuri. Nimeliacha gari mpakani. Tajiri amepeleka dereva mwingine kwa gari ndogo na ndiyo niliyorudi nayo Dar.”
“Umeshakwenda hospitali?”
“Sijakwenda. Nimemeza tu tembe za malaria.”
“Ungekwenda hospitali ili uchukuliwe vipimo, kama ni malaria ieleweke.”
“Nitakwenda kesho asubuhi.”
“Kwanini usubiri kesho asubuhi wakati unaumwa? Hospitali ziko wazi wakati wote. Nenda usiku huu. Usisubiri kesho, je, kama utazidiwa?”
“Sawa, nitakwenda.”
“Utanijulisha itakavyokuwa.”
“Sawa.”
Sufiani akakata simu.
Nikawaza: kesho mume wangu anakuja wakati kuna balaa kama lile. Sijui itakuwaje?
Asubuhi kulipokucha nilijiuliza tena kama niende nikashinde kwa wazazi wangu au nisiende. Nilijiuliza hivyo kwa sababu mume wangu alishanipigia simu usiku na kuniambia angekuja Tanga.
Sasa kama angekuja na kunikuta sipo wakati amenieleza kuwa anaumwa, lingekuwa si jambo zuri.
Nikaamua niende Sahare kuwaeleza wazazi wangu masahibu yaliyonikuta kisha niwahi kurudi nyumbani. Kitu muhimu kilikuwa ni kuwapa wazazi wangu taarifa. Hata kama nitakamatwa watajua nimekamatwa kwa sababu gani.
Nikaondoka pale nyumbani kabla hata ya kuchemsha chai. Jinsi moyo wangu ulivyokuwa umepata fadhaa sikuwa nikisikia njaa wala sikutamani kula chochote.
Nikaenda Sahare kwa bodaboda. Nilipofika, baba alikuwa hayupo. Mama aliniambia baba alikuwa na safari zake mwenyewe.
Baada ya kusalimiana na mama, bila shaka mama alinishitukia kwani aliniuliza, “Unaumwa?”
“Kwanini unaniuliza hivyo?”
“Naona umepauka sana.”
“Ni mambo tu, mama. Nimekuja nikueleze. Ukisikia nimekamatwa au nimefungwa usishangae.”
Kauli ile ikamshitua mama yangu.
“Kwani kumetokea nini?”
Nikamueleza mama ukweli wote. Nilichomficha ni kile kitendo cha kulala na Shefa. Nilimwambia Shefa alikuja kwangu usiku akiwa amelewa na pia alikuwa ananitongoza.
Lakini akapitiwa na usingizi sebuleni. Nilimuamsha; hakuamka, nikamuacha na kwenda kulala. Saa nane usiku nilipoamka ndiyo nikamkuta amekufa karibu na mlango wa choo na karibu yake kukiwa na rungu alilopigiwa.
Nikamwambia mama inawezekana ni mwizi aliyeingia na kumshambulia wakati Shefa anatoka maliwatoni, kwani dirisha lililokuwa kando ya mlango lilikuwa limevunjwa.
Baada ya kumueleza tukio zima lilivyokuwa hadi nilivyokwenda kuutupa mwili wa Shefa na kuonekana na Raisa, mama yangu alishituka na kushangaa.
Alinyamaza kimya kwa karibu dakika nzima akinitazama, kisha akaniuliza, “Hapo ulipoona Shefa amekuja kwako usiku na kukusumbua, kwanini hukumpigia simu mume wako na kumueleza?”
Maswali yakaanzia hapo. Sikuwa hata nimepanga majibu.
“Kama ningemueleza Sufiani, si ningewagombanisha na rafiki yake? Niliona nimuache tu.”
“Unajua kosa lako ni nini?”
“Niambie nilichokosea.”
“Baada ya kuona huyo mtu ameuawa, ungepiga simu polisi na kuwaeleza ukweli, lakini wewe hukufanya hivyo. Ule mzigo ukaufanya ni wako wewe.”
“Sasa mama, hebu fikiria mwenyewe: mimi mke wa mtu, Shefa mume wa mtu, anakutwa ameuawa nyumbani kwangu usiku wa manane — nitaelewekaje?”
“Lakini aliyekuponza ni yeye. Hakuwa mtu mzuri; amekutafutia balaa la bure, mwanangu.”
“Ndiyo, nimekuja kukuambia. Mkisikia nimekamatwa kwa sababu ni hiyo…”
“Sasa utafanyaje mwanangu ujinusuru na hilo tatizo?”
 “Ndiyo nimekuja kuwaeleza, labda mtanipa wazo.”
 “Raisa ni rafiki yako pete na chanda, kwanini usimuite ukamueleza ukweli ili awe upande wako.”
 “Ilitakiwa nimueleze tangu mapema. Kama nilimficha siwezi kumueleza tena. Na yeye ndiye kidomo domo mkubwa.”
 “Amekuwa kidomodomo kwa sababu hajui kama wewe shoga yake ndiye uliyehusika. Hilo nalo ni kosa jingine ulilolifanya. Sasa  mwenzako anatafuta namba za gari lililotupa huo  mwili, unafikiri akijagundua ni garilako wakati ulimficha si atajua wewe ndiye muuaji! Patakuwa  na urafiki tena hapo?”