Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Lissu aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo, Septemba 8, 2025 akihoji endapo Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam ina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhaini.
Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 15, 2025 na kiongozi wa jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru baada ya kupitia hoja za mshtakiwa na upande wa mashtaka.
Jaji Ndunguru amesema pingamizi lililowasilisha na Lissu halina mashiko na kwamba Mahakama hiyo inalitupilia mbali.
Baada ya kutoa uamuzi huo, upande wa mshtaka ukiongozwa na Nassoro Katuga umeiomba Mahakama hiyo impatie nyaraka zote ambazo alizilalamikia kuwa hajapewa.
Jaji Ndunguru alikubaliana na ombi la Katuga na kuelekeza nyaraka alizoomba mshtakiwa huyo zikiwamo za viapo vya kulinda mashahidi.
Baada ya kutoa maelekezo hayo, Jaji Ndunguru ameahirisha kesi hiyo hadi saa 8:00 mchana, itaendelea wa upande wa mashtaka kumsomea hati ya mashtaka mshtakiwa huyo.
Endelea kufuatilia mtandao wa Mwananchi