Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/26 unakaribia kuanza rasmi huku mashabiki, wadau wa soka na wanamichezo kwa ujumla wakisubiri kwa hamu kuona kile ambacho klabu zao zitakifanya.
Pia kuna jambo moja muhimu ambalo bado limeacha maswali mengi bila majibu tuzo za wachezaji bora wa msimu uliopita (2024/25), haijajulikana kama zitakuwepo au hazitakuwepo kwani bado hazijatangazwa.
Kwa kawaida, baada ya kila msimu wa Ligi Kuu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi (TPLB) limekuwa likitoa tuzo mbalimbali kwa ajili ya kutambua mafanikio na mchango wa wachezaji, makocha, waamuzi na timu mbalimbali zilizofanya vizuri.
Lakini hadi leo, ikiwa ni siku chache kabla ya msimu mpya kuanza, bado haijajulikana ni lini tuzo hizo zitatolewa, nani atashinda, wala hata kama tukio hilo lipo kwenye ratiba rasmi.
Katika msimu wa 2024/25, ushindani ulikuwa mkubwa. Yanga iliendelea kutawala soka la Tanzania kwa kutetea taji la Ligi Kuu Barapamoja na Kombe la FA.
Kwa upande wa wachezaji binafsi, kulikuwa na mastaa waliovutia mno na katika mbio za kiatu cha dhahabu, Jean Charles Ahoua wa Simba aling’ara kwa mabao yake 16.
Katika lango, Moussa Camara wa Simba alimaliza msimu na clean sheets 19, akifuatiwa na Djigui Diarra (17) na Patrick Munthari (15) na walionyesha viwango vizuri ikiwamo kuokoa mabao na hivyo kuongeza mvuto katika uwaniaji wa tuzo kwa miaka ya karibuni.
Ni wazi vigezo vya utoaji wa tuzo vipo wazi na wengi wanajiuliza kwa nini zimechelewa, au hazipo na hapa ndipo wahusika wanatakiwa wawe wawazi ili wadau na mashabiki wajue.
Licha ya kuwepo na mambo mengine yaliyoingia baada ya ligi kumalizika ikiwamo michuano ya Chan, kufuzu kombe la dunia, uchaguzi wa TFF na michuano ya Kombe la Kagame lakini jambo hili lilitakiwa liwe katika ratiba za baada ya msimu kwani ni la siku moja na hivyo kamati inaweza kuendelea na maandalizi yake wakati mambo mengine yanaendelea.
Imeshawahi kutokea mara kadhaa wachezaji na hata makocha wanatajwa kuchukua tuzo na hawapo nchini na kupokelewa na watu wao wa karibu.
Hii inapoteza mvuto kwani ni muhimu mhusika awepo katika sherehe hizo kufurahi mafanikio ya msimu na wenzake kabla ya kutawanyika.
Tunaamini tuzo hizi zitakuwepo na kamati ya waandaaji inaendelea kukamilisha ili zitangazwe zitafanyika lini ingawa kwa kuchelea na misimu inayofuata zifanyike mapema ili kuongeza mvuto..
Zinaweza pia kuwekwa katika ratiba ya msimu ili ijulikane mara baada ya msimu kumalizika, utoaji wa tuzo utafanyika lini na wahusika wawe wamejiandaa kutokana na ratiba hiyo na si kushtukizwa wakati wameshaondoka nchini.