Vilevile WMA Dodoma imetoa wito kwa wafanyabiashara hao kwa upande wao kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi na kwa usahihi ili kuwezesha wanunuzi kupata bidhaa stahiki kulingana na kiasi cha fedha wanacholipa.
Wito huo umetolewa Septemba 13, 2025 na Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi alipokuwa akizungumza katika semina ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara wanaounda Umoja wa wenye Viwanda vya Alizeti Kongwa (UVAKO).
“Mji wa Kibaigwa ni miongoni mwa miji mikubwa yenye mzunguko mkubwa wa biashara na una idadi kubwa ya vipimo vinavyotumika katika eneo hili, Jukumu kuu la WMA ni kusimamia usahihi wa vipimo hivyo tutaendelea kufanya kaguzi za vipimo kila mara kama Sheria ya Vipimo Sura 340 inavyoelekeza kwa lengo la kuhakikisha biashara zinafanyika kwa haki pasipo upande wowote kupunjika,” alisema Meneja Zuberi.
Kwa upande wake, akiwasilisha mada wakati wa semina hiyo, Afisa Vipimo Mwandamizi Bw. Saidi Ibrahimu aliwataka wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya alizeti kuhakikisha mizani inayotumiwa kununua na kuuza zao la alizeti imehakikiwa na WMA na imebandikwa stika inayoonyesha tarehe mzani ulipokaguliwa na tarehe ambayo utatakiwa kuhakikiwa tena.
Pia, aliwataka wafanyabiashara watakao ongeza thamani ya zao la alizeti kwa kukamua mafuta ya alizeti na kuyafungasha wazingatie matumizi sahihi ya vipimo kwa kuweka ujazo sahihi wa bidhaa hiyo kwenye vifungashio ili waepuke kujipunja au kuwapunja wanunuzi wa bidhaa hiyo.
“Unapufungasha bidhaa, kuna mambo muhimu ya kuzingatia ikiwa ni pamoja na kuweka jina la utambulisho wa bidhaa, jina na mahali unapofanyia ufungashaji, weka anuani ya posta, simu au barua pepe kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano pamoja na kuandika kiasi cha bidhaa kilichofungashwa kwenye kifungashio na kuweka alama ya ujazo, uzito au urefu wa bidhaa mfano 200 kg”, alifafanua.
Naye Mwenyekiti UVAKO, Bw. Clement Sangale aliishukuru na kuipongeza WMA kwa kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo akisema ilikuwa ni shauku yao kwa muda mrefu hususani kuelimishwa kuhusu Sheria ya Vipimo Sura 340 kwa lengo la kuifahamu ikiwa ni pamoja na kufahamu ada mbalimbali zinazotozwa na WMA.
“Semina hii imekuwa na manufaa makubwa kwa wajumbe wa UVAKO ambapo pamoja na mengine mengi tumefahamu haki na wajibu wetu kama wafanyabiashara, hivyo tunaahidi kuendelea kutii sheria bila shuruti kwa kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo yetu ya biashara,” alisema Mwenyekiti.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi, alibainisha kuwa mojawapo ya majukumu ya WMA ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya vipimo, hivyo alisema kuwa elimu hiyo itaendelea kutolewa katika makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wakulima na wananchi kwa ujumla.
Aliongeza kusema kuwa, kwa sasa elimu ya vipimo itaelekezwa pia kwenye shule mbalimbali za Msingi na Sekondari katika kuhakikisha wanafunzi wanapata uelewa mzuri wa matumizi sahihi ya vipimo na kwamba litakuwa ni zoezi endelevu.