Kesho macho yote yataelekezwa kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo watani wa jadi Simba SC na Young Africans SC watakutana katika Ngao ya Jamii, mchezo unaozindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, ameweka wazi kuwa timu yake inatazamia kuanza msimu kwa kishindo, akisema wachezaji wake wamejaa shauku kubwa ya kuwaridhisha mashabiki. “Tunataka kutoa matokeo mazuri ili mashabiki wapate kile wanachotarajia. Hii ni derby kubwa, lazima tuanze na nguvu,” alisema Folz.

Kwa upande mwingine, nahodha mpya wa Simba, Shomary Kapombe, amewataka wachezaji wapya kuelewa uzito wa mechi hii ya Kariakoo Derby. “Tumewaeleza wachezaji wapya umuhimu wa mchezo huu. Ngao ya Jamii si mechi ya kawaida – ni heshima, ni fahari, na ni moyo wa mashabiki,” alisema Kapombe.
Mchezo huu si wa pointi pekee, bali ni kipimo cha nguvu, mbinu, na heshima. Mashabiki wa pande zote mbili wanasubiri kuona nani ataandika ukurasa mpya wa historia ya Kariakoo Derby 2025.
Related