Jeshi la Polisi Lamuita Polepole Kutoa Ushahidi wa Tuhuma – Global Publishers



Jeshi la Polisi limetangaza kuwa linafanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma za makosa ya kijinai zilizotolewa na Humphrey Herson Polepole. Tuhuma hizo, kama zilivyoelezwa na mhusika kupitia mitandao ya kijamii, zinahitaji ushahidi wa kuthibitisha zitakapo wasilishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi limesema kwamba, baada ya kufungua jalada na kuanza uchunguzi, limeendelea kukusanya ushahidi na kufanya jitihada za kumpata mhusika ili aweze kutoa maelezo, ushahidi na vielelezo vitakavyothibitisha tuhuma hizo. Hii itasaidia kurahisisha hatua za kisheria kufuatia taratibu zilizowekwa na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Bwana Polepole ameelekezwa kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili kutoa maelezo na ushahidi kuhusiana na tuhuma hizo. Jeshi la Polisi linasisitiza kuwa ufuatiliaji huu unafanywa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi ameongeza kuwa jitihada za kukusanya ushahidi na maelezo kutoka kwa mhusika zinaendelea, ili kuhakikisha kwamba haki inatimizwa kwa mujibu wa sheria.