Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Soko la Kawe jijini Dar es Salaam, wamejikuta wakilala kwa majonzi baada ya soko hilo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo, Jumatatu, Agosti 15, 2025, na kusababisha upotevu wa mali.
Moto huo ambao chanzo chake hakijajulikana, umeteketeza bidhaa mbalimbali walizokuwa wakitegemea kulipia mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Tukio hilo limewaacha wafanyabiashara wengi katika hali ya taharuki huku wakieleza kuwa, maisha yao yako shakani bila msaada wa haraka.
“Tumepoteza kila kitu. Bidhaa zote tulizokuwa tunauza zimeungua. Hatuna pa kuanzia tena bila msaada wa Serikali,” amesema mmoja wa wafanyabiashara waliokuwa wakihangaika kutazama mabaki ya bidhaa zake zilizogeuka majivu.

Wengi wao wamesema walikuwa wakitegemea mapato kutoka sokoni hapo kulipa mikopo, jambo linalowaweka katika hatari ya kushindwa kurejesha madeni na kuathiri familia zao.
Hamis Walid, mfanyabiashara sokoni hapo amesema eneo analofanyia biashara hakuna kilichosalia na sasa hajui cha kufanya kwa kutokuelewa pa kuanzia huku akiiomba Serikali kuwasidia ili kurejesha mikopo waliyochukua.
“Asilimia kubwa ya wafanyabiashara humu ndani tunaishi kwa mikopo na huo ndiyo ukweli, tunaomba kama tutapata mkopo hata ya gharama nafuu kutoka serikalini itakayotufanya kuweza kurejesha ile ya awali kwa kulipa kidogo kidogo kwao,” amesema Walid.
Hadi sasa, mamlaka husika bado hazijatoa taarifa rasmi kuhusu kilichosababisha moto huo, huku jitihada za uchunguzi zikiwa zimeanza kubaini kiini cha janga hilo.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na wafanyabiashara na wananchi waliokuwepo katika eneo la soko la Kawe ambalo limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo
Mfanyabiashara wa soko hilo, Deus Mkude amesimulia namna walivyopata taarifa: “Nilipata taarifa za moto nikiwa nyumbani, nikakimbia haraka kuja sokoni kuona kama nitaweza kuokoa kitu. Lakini nilipofika, moto ulikuwa umesambaa sana hatukuweza kuokoa chochote.”
Amesema vibanda vyao vilivyojengwa kwa mbao na mabati vilishika moto kwa haraka na juhudi za kuzima zilikuwa ngumu kutokana na upungufu wa maji.
“Gari la Zimamoto lilifika, lakini maji yalikuwa kidogo, walijaribu kuzima yakaisha wakaondoka kuchukua mengine. Moto ulikuwa mkubwa, ukasambaa hadi majengo mengine,” amesimulia mfanyabiashara huyo.
Mkude ameeleza kuwa, hasara ni kubwa kwa sababu kila kitu kimeteketea na hakuna aliyeokoa mali na hakuna mfanyabiashara ambaye amekata bima.
Naye, Zawadi Kimaro mfanyabiashara wa kuku ameomba waruhusiwe kufanya biashara kutokana na biashara wanayoifanya, isijekuathirika na kupata hasara.
“Japokuwa upande wa kuku moto haujafika, lakini tumezuiwa kuendelea na biashara, tunachoomba turuhusiwe kuendelea maana wateja wanakuja, lakini hatuwezi kufanya chochote,” amesema Zawadi.
Amelalamikia pia kuibwa kwa kuku waliotolewa kwenye banda ili kuwanusuru na moto huo, lakini wamejitokeza watu wakawaiba.
Halmashauri kutoa Sh100 milioni
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza mpango wa muda mfupi na mrefu kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara waliopoteza mali na kuhakikisha soko hilo linajengwa upya kwa viwango vya kisasa.
Katika hatua za dharura, Chalamila amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Suleiman, kutoa Sh100 milioni kwa ajili ya kuwafariji na kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika.

“Ni lazima tufikirie namna ya kuwasaidia wenzetu waliopata hasara. Serikali imetenga Sh100 milioni kwa dharura hii, lakini pia tutaangalia ili kila mmoja apate angalau kidogo cha kumsaidia kuanza upya. Hii fedha si ya mtu mmoja, ni kwa ajili ya wote walioathirika,” amesema Chalamila.
Amesema fedha hizo zitatolewa kwa uwazi ili kuhakikisha kila mfanyabiashara aliyepoteza mali ananufaika.
Aidha, ameagiza wafanyabiashara wote walioathirika kuhamia kwa muda katika eneo la Tanganyika Packers kupisha maandalizi ya ujenzi mpya wa soko hilo.
“Kwa sababu ya dharura hii, wafanyabiashara waliopata athari wahamishwe mara moja kwenye eneo la Tanganyika Packers. Hapa hatuwezi kukarabati wakati watu wako ndani, lazima tuanze maandalizi mapema. Mkurugenzi hakikisha sheds zinajengwa kwa haraka,” ameongeza.
Chalamila amesema eneo la Kawe ni la kimkakati na haliwezi kuendelea kuwa na mabanda ya muda yasiyo na ubora, hivyo ameagiza ramani ya soko jipya ikamilike mapema na ujenzi uanza mara moja.
“Soko hili lazima lijengwe upya kwa haraka na liwe la kisasa. Sio hivi vibanda vibanda. Eneo la Kawe ni muhimu, hatuwezi kuliacha hovyo. Mkurugenzi niletee ramani ya soko hili mapema ili tuanze kujenga vizuri,” amesema.
Bima kuwa sharti la kurejea sokoni
Aidha, Chalamila ameeleza changamoto kubwa inayojitokeza kila mara masoko yanapoungua moto ni ukosefu wa bima kwa wafanyabiashara.
Hivyo, ameweka wazi kwamba, kabla ya mfanyabiashara yeyote kurudi sokoni baada ya ujenzi mpya, ni lazima awe na bima.
“Kabla ya mfanyabiashara kuingia tena sokoni hapa, lazima awe na bima. Kama bima ingekuwepo leo, wafanyabiashara wote wangelipwa fidia. Hili lazima liwe somo. Kama tulivyofanya Kariakoo, hapa pia hatutaruhusu mtu yeyote kuanza biashara bila kuwa na bima ya moto,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Amesema mchanganyiko pia wa biashara alizoziita kuwa za hatari zilizokuwa zinafanyika sokoni hapo, zimechangia moto huo kusambaa kwa haraka.
Chalamila amesema alipita ndani ya soko na kushuhudia biashara za gesi, kuni na mkaa zikifanyika sambamba na wapishi wa chipsi na vyakula, hali ambayo ni hatari kwa usalama wa wote.
“Nimezunguka sokoni, nimekuta wanauza gesi, kuni, mkaa na huku pembeni wanapika chipsi. Ni wazi moto unapotokea uharibifu unakuwa mkubwa zaidi. Mkurugenzi hakikisha biashara hizi zinawekwa kwa mpangilio sahihi, sio katikati ya soko,” amesema Chalamila.
Aidha, Chalamila ametoa onyo kwa watu wanaodaiwa kuiba mali za wafanyabiashara hao badala ya kusaidia kuziokoa.
“Nimepewa taarifa kuwa badala ya kuokoa mali za wafanyabiashara, watu wengine wameiba mali hizo, huku baadhi yao wakiwa wanawake, jambo ambalo si la kawaida na halikubaliki,” amesema kwa msisitizo.

Wakati Chalamila akisema hivyo, mmoja ya wazee wanaoishi jirani na soko hilo, Yusufu Abdallah maarufu Mzee Sasi amewataka wale wote waliochukua mali za watu kurudisha kabla ya kusomwa kwa dua.
“Niombe kitu kimoja, wale wote waliochukua mali ambazo sio za kwao wazirudishe kabla ya kusomwa kwa dua,” amesema Sasi.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Jacob Chacha amesema atatoa taarifa baadaye kuhusiana na tukio hilo.
“Bado tupo kwenye tathmini, tutatoa taarifa maana nilikuwa kwenye kikao,” amesema Chacha.