Lissu akwama hatua ya kwanza pingamizi kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekwama katika hatua ya kwanza ya kujinasua katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, kutupilia mbali sababu yake moja ya pingamizi lake.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Katika uamuzi huo uliotolewa leo, Jumatatu, Septemba 15, 2025, Mahakama imeitupilia mbali sababu hiyo baada ya kukataa hoja zake zote, huku ikisema kuwa ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

“Mahakama baada ya kupitia hoja za pande zote imeridhika kuwa mapingamizi haya hayawezi kuharibu mwenendo mzima wa Mahakama ya Ukabidhi na kuifanya Mahakama hii kukosa mamlaka. Hivyo sababu hii ya pingamizi inakataliwa,” amesema Jaji Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo)  wakati akisoma uamuzi huo baada ya kujadili hoja zote. Majaji wengine wanaosikiliza kesi hiyo ni James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.


Kwa uamuzi huo, Mahakama hiyo imepanga kuendelea na usikilizaji wa sababu ya pili ya pingamizi la Lissu, inayohusu uhalali wa hati ya mashtaka, kuanzia saa 8:00 mchana.

Hoja za pingamizi la Lissu

Katika pingamizi lake hilo, Lissu alidai kuwa Mahakama hiyo (Mahakama Kuu) haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo huku akibainisha hoja saba.

Hoja hizo alizodai zinaifanya Mahakama hiyo kukosa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ni pamoja na ubatili wa mwenendo kabidhi na mamlaka ya Mahakama ya Ukabidhi.

Mamlaka ya Mahakama ya Ukabidhi

Lissu alidai kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa kwanza imepelekwa hapo kutoka katika Mahakama ya Ukabidhi (Committal Court), ambayo haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza katika hatua ya ukabidhi.

Alifafanua kuwa Mahakama ya Kisutu iliyoendesha mwenendo kabidhi haikuwa na mamlaka hayo kisheria, kwani mwenendo huo ulipaswa kuendeshwa na Mahakama ya mahali alikokamatwa, yaani Mbinga, mkoani Ruvuma, kama sheria inavyoelekeza, na si kosa linakodaiwa kutendeka.

Jamhuri kupitia jopo la mawakili wa Serikali, linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, lilijibu madai yake hayo hayana mashiko.


Kuhusu kutokushtakiwa alikokamatwa Mbinga, mkoani Ruvuma, Wakili Katuga alidai kuwa mtu anashtakiwa katika Mahakama ya mahali alikofanyia kosa, na kwamba japo alikamatwa Mbinga, lakini kosa anadaiwa kulifanyia Dar es Salaam.

Mahakama katika uamuzi wake imekubaliana na hoja za Jamhuri kuwa Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka kamili ya kusikiliza kesi hiyo katika hatua ya awali, yaani ukabidhi.

Ubatili wa mwenendo kabidhi

Mwenendo kabidhi (committal proceedings), ni mwenendo wa uhamishaji kesi kutoka Mahakama ya chini na kuikabidhi Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza.

Lissu alidai kuwa mwenendo kabidhi huo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni batili, kwani uliendeshwa bila kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023, vifungu vya 263, 264, 265 na 266 vinavyohusiana na mwenendo kabidhi.

Ukiukwaji huo wa sheria alioudai Lissu ni pamoja na kesi kuahirishwa mara 13 bila kutoa sababu za msingi na kwamba ilitoa sababu mara tatu pekee.

Hata hivyo, Jaji Ndunguru amesema kuwa Mahakama ya Ukabidhi (Kisutu) ilikuwa na wajibu wa kumsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo na kuihamishia Mahakama yenye mamlaka ya kuisikiliza (Mahakama Kuu), na kwamba Mahakama hiyo ya Ukabidhi ina ukomo wa kushughulikia kesi hiyo.


Jaji Ndunguru amesema Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kuandika maelezo mengine zaidi ya kuahirishwa kwa kesi na kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi na kuiahamishia Mahakama Kuu.

“Hivyo, Mahakama hii inaona madai ya kuahirisha kesi bila kutoa sababu hayawezi kumnyima mshtakiwa haki ya msingi,” amesema Jaji Ndunguru.

Kuhusu madai ya Mahakama ya Ukabidhi kukiuka uamuzi na amri ya Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi, Mahakama hiyo imesema kuwa baada ya kupitia yaliyoendelea katika Mahakama ya Ukabidhi, imeona kuwa haijapingana na amri ya Mahakama Kuu.

Kuhusu madai ya Lissu kutokupewa baadhi ya nyaraka za mwenendo kabidhi, Mahakama hiyo imesema ingawa alikuwa na haki ya kupewa nyaraka hizo bila malipo, lakini ikakubaliana na Jamhuri kuwa kutokupewa nyaraka hizo katika Mahakama ya Ukabidhi bado hakumcheleweshi kwa kuwa bado usikilizwaji (trial).

Kuhusu madai ya Mahakama kutokurekodi baadhi ya taarifa na mashahidi wa mshtakiwa kutokuorodheshwa na kutokusaini kumbukumbu za mwenendo, sheria inatoa hiyari kusaini au kutokusaini, na kwamba ingawa hakusaini, lakini haioneshi kwamba alikataliwa.

Hivyo, Mahakama hiyo imesema kuwa kwa kuwa hiyo ni hiyari, haioni kama kutosaini kuna haribu kumbukumbu.

Kuhusu madai Mahakama kumkatalia kuorodhesha majina ya mashahidi wake aliowataja Samia Suluhu Hassan, Dk Phillip Mpango na Kassim Majaliwa, pia Mahakama hiyo imeyakataa.

Mahakama imesema kuwa Mahakama ya Ukabidhi (Kisutu) ilifanya hivyo kwa kusingatia ukomo wa mamlaka yake, kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kufanya mwenendo wa ukabidhi.

Jaji Ndunguru amesema kutokuorodheshwa kwa mashahidi wake kwenye mwenendo kabidhi hakuufanyi kuwa batili, na kwamba chini ya kifungu cha 181 na 314(1) vya CPA vinampa nafasi ya kuita mashahidi wake wakati kesi itakapoanza kusikilizwa (trial).

Kuhusu madai ya kuwepo viashiria vya kughushi nyaraka kwa madai ya kupewa kumbukumbu za mwenendo kabidhi tofauti na zilizoko mahakamani, pia Mahakama hiyo imeyakataa.

Jaji Ndunguru amesema kuwa madai hayo yanahitaji ushahidi, na kwamba Mahakama imeona ni vyema isishughulikie nalo isipokuwa hoja za mamlaka ya Mahakama.

Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Kisutu, ilikofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza.

Katika kesi hiyo, Lissu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.