Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha semina maalum kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, ikiwa na lengo la kutoa elimu, kuongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma katika kuhabarisha jamii kuhusu majukumu ya Bodi hiyo.
Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, amesema kuwa NBAA imejikita katika kukuza taaluma ya Uhasibu kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha taaluma hiyo inatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa na bara la Afrika kwa ujumla.
“Vyombo vya habari ni daraja muhimu kati ya taasisi kama NBAA na wananchi. Ushirikiano wetu utasaidia kuongeza uelewa kuhusu taaluma ya Uhasibu na nafasi yake katika uchumi wa nchi,” amesema CPA. Maneno.
CPA. Maneno alieleza kuwa NBAA inatambua nafasi ya vyombo vya habari kama wadau wakuu wa kutoa elimu kwa umma, hasa kuhusu masuala ya fedha, taarifa za ukaguzi na uendeshaji wa Taasisi kwa uwazi na uwajibikaji. Alibainisha kuwa kwa sasa NBAA inatoa huduma zake zote kidijitali kama vile usajili wa wanafunzi na wanachama, ulipaji wa ada, usajili wa kampuni za Kihasibu na Kikaguzi n.k kwa kutumia mifumo inayopatikana kupitia tovuti ya NBAA.
Katika kuendeleza uelewa wa taaluma hiyo, CPA. Maneno aliwataka waandishi wa habari kushirikiana kwa karibu na NBAA katika kuhakikisha taarifa sahihi za kitaaluma zinawafikia jamii kwa wakati.
“Tunahitaji ushirikiano wa karibu na nyinyi wana habari. Kupitia kalamu zenu, jamii itaweza kuelewa nafasi ya Uhasibu katika maendeleo ya Taifa,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA, CPA Kulwa Malendeja, alieleza kuwa mojawapo ya majukumu ya msingi ya Bodi hiyo ni kusimamia Taaluma ya Uhasibu nchini. Amesema wahasibu wote waliomaliza ngazi ya juu ya kitaaluma yaani CPA usajiliwa na NBAA.
Kwa upande mwingine, NBAA imewahakikishia wanahabari kuwa itaendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kutoa elimu kwa jamii juu ya nafasi ya Taaluma ya Uhasibu na umuhimu wa kuwa na taarifa za kifedha zilizo sahihi zilizokaguliwa na kuthibitishwa kitaalamu.
“Tunaishukuru sana tasnia ya habari kwa ushirikiano wenu. Tunaamini kupitia ninyi, jamii ya Watanzania itaendelea kupata uelewa wa kina kuhusu majukumu ya NBAA pamoja na taarifa mbalimbali za fedha zinazotolewa na Taasisi tofauti,” amesema CPA Malendeja.
Semina hiyo ni sehemu ya mikakati ya NBAA ya kuimarisha mawasiliano ya Taasisi hiyo kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha waajiri kuhakikisha wanatumia wahasibu waliobobea na waliosajiliwa rasmi na Bodi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno akizungumza kwa njia ya mtandao kwenye semina maalum kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo Peter Lyimo akizungumzia kazi zinazofanywa na kurugenzi hiyo kwenye semina maalum kwa wahariri na waandishi wa habari.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya akitoa ufafanuzi kuhusu kazi zinazofanywa na bodi hiyo wakati wa semina maalum kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.