Kabutali kuanza kampeni wiki ijayo, aahidi kumaliza migogoro ya ardhi Mtumba

Dodoma. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Kayumbo Kabutali, ametangaza kuzindua kampeni zake Septemba 25, 2025, akieleza kuwa anakwenda kuchukua jimbo asubuhi, kwani siku zilizobaki kwa ajili ya kampeni zinamtosha.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, alipoulizwa kwa nini hajaanza kampeni wakati pazia lake lilishafunguliwa tangu Agosti 28, 2025 na wagombea wengine wa chama hicho, ikiwemo madiwani, wanaendelea na kampeni katika jimbo hilo.

Hii ni mara ya tatu kwa Kayumbo kugombea nafasi hiyo. Mara moja aligombea kupitia NCCR-Mageuzi, na uchaguzi uliopita aligombea kwa tiketi ya Chaumma akiwa Makamu Mwenyekiti wa chama Taifa, lakini hakufanya kampeni zaidi ya kutuma sera zake kwenye mitandao, huku akimnadi mgombea urais wa wakati huo, Hashim Rungwe.

Amesema bado hajachelewa kwani jimbo la Mtumba lina Kata 20, na anaamini muda huo unamtosha kufika kila kata na kuzungumza na wananchi ambao wana hamu ya kuwa na mbunge mpya.

Mgombea huyo ameeleza baadhi ya mambo ambayo angetamani kuanza nayo, ikiwemo kilio cha wakazi wa jimbo hilo ni kupambana kuondoa migogoro, kuongeza upatikanaji wa maji kwa kufufua visima virefu vya Mzakwe ambavyo awali vilikuwa 22 lakini sasa vinatoa maji visima vinane pekee.

Akijibu hoja za kama ataendelea kufanya kampeni kwa njia ya mtandao kama alivyofanya mwaka 2020, amesema kwenye uchaguzi wa mwaka huu atakwenda kila kata na mitaa, kwani chama kimekuwa tofauti na ilivyokuwa mwaka 2020.

Ameeleza kuwa anakwenda kuwachongea CCM kwa wananchi namna walivyosababisha migogoro ya ardhi hadi wilaya ikawa kinara kwa migogoro hiyo nchi nzima.