Unguja. Zaidi ya wanachama 450 wa chama cha ACT Wazalendo wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakieleza kuvutiwa na uongozi bora wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Wanachama hao wamepokewa leo, Septemba 15, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni kwa Pemba katika Viwanja vya Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba.
Idadi ya wanachama hao imetajwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, akisema wameamua kuunga mkono chama hicho kutokana na maendeleo yaliyofanyika.
Mwakilishi wa kundi hilo, aliyekuwa Mjumbe wa ngome ya ACT Wazalendo kutoka Micheweni, Faki Ali Juma, amesema wameamua kwa hiari yao kujiunga na CCM baada ya kushuhudia kasi ya maendeleo na dira ya uongozi wa Dk Mwinyi, akisisitiza kuwa chama hicho ndicho kinachoonesha mwelekeo wa kweli wa kuijenga Zanzibar.
“Tumevutiwa na uongozi wake, ndiyo maana tumeamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi,” amesema Faki.
Ameahidi kuwa watapiga kura nyingi ifikapo Oktoba 29 na kuhamasisha wengine wawapigie kura wagombea kutoka CCM.
Amesema kuwa wamejiwekea mkakati wa kuhakikisha wanahamasisha kila mmoja, wakiwemo wagombea wengine kutoka vyama vingine, kikiwemo chama walichotoka cha ACT.