………………………
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
15/09/2025 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa shilingi milioni 250 kutoka kwa BAPS Charity Tanzania fedha zitatumika kulipia matibabu ya moyo ya watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.
Akipokea msaada huo jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwashukuru BAPS Charity kwa kujitoa kwao kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema tangu mwa 2015 BAPS Charity wamekuwa washirika wakubwa wa taasisi hiyo kutokana na fedha wanazozitoa ambazo zimesaidia kuokoa maisha ya watoto, kutoa elimu na mafunzo kwa madaktari.
“Mchango wa BAPS Charity umechangia kuifanya taasisi yetu kuwa moja ya Taasisi bora Afrika Mashariki na Kati na kuwa taasisi ya tatu Afrika ambayo inatibu magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima”.
“Mchango wao siyo tu fedha bali unasaidia kuokoa vifo vya watoto, unajenga taifa la kesho na kujenga Tanzania mpya”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mratibu wa BAPS Charity Tanzania Kapil Dave alisema msaada huo unalenga kusaidia kutibu watoto wenye matatizo ya moyo na kupunguza safari za nje ya nchi kwenda kupata matibabu.
“Tumeungana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwaka 2018 katika kuokoa maisha ya watoto 450 wenye matatizo ya moyo, ninawaomba watanzania wengine wajitokeze kuiunga mkono Serikali kutoa msaada hapa JKCI ili watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kiuchumi waweze kupata matibabu”, alisema Dave.
Mwisho