Dar es Salaam. Huenda upikaji wa taarifa za hesabu za fedha unaofanywa na baadhi ya taasisi na wafanyabiashara ukafikia tamati baada ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), kuja na mfumo utakakaodhibiti suala hilo.
Hiyo ni kwa sababu sasa itakuwa lazima kwa taarifa zote za fedha zilizokaguliwa kuwekwa katika mfumo wa NBAA Verification Number (NBAAVN) utakaofanya kila taarifa kupewa namba maalumu inayoweza kutumika katika maeneo tofauti ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na benki mbalimbali za biashara.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Septemba 15, 2025, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na NBAA ikielezea mikakati inayofanywa na benki hiyo ili kuhakikisha taaluma hiyo haivamiwi na vishoka watakaoharibu fani.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Viwango vya Kiuhasibu, Utafiti na Ufundi, Angyelile Tende amesema upikaji wa hesabu ulikuwa ukiwanufaisha walengwa huku ukisababisha kupotea kwa mapato ya Serikali sambamba na benki kupata hasara.
Hali hiyo ilisababishwa na watu kuwa na taarifa za hesabu hata tatu tofauti kulingana na matumizi wanayotaka kuyafanya badala ya kuwa na moja pekee.
“Unakuta mtu ana taarifa kwa ajili ya benki ambayo inaonesha anapata faida sana wakati kiuhalisia anapata hasara au anawapa taarifa Mamlaka ya Mapato inaoonesha kuwa amepata faida kidogo wakati amepata faida kubwa hii inafanya kodi anayolipa inakuwa ndogo,” amesema.
Amesema kwa wale ambao hupeleka benki taarifa zisizokuwa za kweli wamekuwa wakisababisha hasara kwa kuwa, wanakopesha kampuni au wafanyabiashara ambao hawana uwezo wa kulipa madeni yao kutokana na kutotengeneza faida.
“Hali hii ndiyo imefanya kuwapo mwa mikopo chechefu katika benki kwa sababu benki ikishapewa taarifa ilikuwa inakosa sehemu ya kwenda kuthibitisha kama ni za kweli,” amesema.
Akieleze mfumo huo utakavyokuwa ukifanya kazi, Tende amesema hesabu yoyote itakapokuwa ikiandaliwa itakuwa ni lazima kuwekwa katika mfumo huo utakaokuwa unaweza kufikiwa na mtu yeyote anayehitaji kujua uhalali wa hesabau hizo.
Taarifa hizo zitakapochapishwa katika mfumo, TRA, benki na hata wawekezaji watakuwa wanaweza kuzifikia kupitia namba maalumu itakayotolewa kwa kila taarifa ya fedha.
Amesema uwepo wa mfumo huo pia, utasaidia kuondoa vishoka wanaofanya kazi hizo bila kuwa na vigezo maalumu vinavyotakiwa kwa kuwa, ili taarifa itambuliwe na NBAA lazima mkaguzi awe amesajiliwa ili aweze kutoa huduma na kuweka taarifa hizo katika mfumo.
“Kama NBAA kwa kutambua hili kupitia marekebisho ya Sheria ya Uanzishaji NBAA moja ya jambo lililoongezwa ilikuwa ni taarifa zote zilizokaguliwa kuletwa NBAA na sisi kupitia maendeleo ya sayansi na teknolojia ndiyo tumeamua kuja na mfumo huu,” amesema.
Amesema kupitia mfumo huo ni ngumu vishoka kuendelea kufanya kazi kwa kuwa, ni lazima uwe umesajiliwa kama mhasibu au mkaguzi wa hesabu ili uweze kuingiza taarifa za fedha katika mfumo.
“Hivyo, niwaambie tu, zile taarifa za kuandaliwa na vishoka au zimepikwa sasa unakwenda kuisha kupitia mfumo huu wa NBAAVN,” amesema.
Akizungumza namna ambavyo wanalinda taaluma hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, CPA Kulwa Emmanuel Malendeja amesema mara zote wamekuwa wakiwashughulikia wanaobainika kufanya vitendo kinyume na taaluma hiyo ikiwamo udanganyifu au wizi.
“Zipo hatua mbalimbali zinazochukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwamo faini, kufutwa kwa kampuni ya ukaguzi, kufutiwa cheti kwa mgakuzi husika au kusimamishwa kufanya kazi kwa muda fulani, hii imeenda sambamba na kuwafundisha wananchi namna ya kumtambua mkaguzi au mhasibu asiyekuwa kishoka,” amesema.
Mbali na hilo, NBAA wamekuwa wakihakikisha wataalamu wote wanasajiliwa na kulipa ada zao sambamba na kuwapa leseni kila mwaka.
Hilo linaenda sambamba na kuendelea kutolewa kwa mafunzo kazini kwa watu wataalamu wote waliosajiliwa ili kuhakikisha wanaenda sambamba na mabadiliko ya kasi ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani.
Akielezea moja ya changamoto inayolalamikiwa ya watu wengi kufeli mitihani ya maalumu ya utambuzi (CPA), Malendeja amesema moja ya sababu iliyobainika ni watu kukosa maandalizi ya kutosha.