Joshua Ibrahim ajipanga upyaa Fountain

MSHAMBULIAJI mpya wa Fountain Gate, Joshua Ibrahim amesema baada ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja, atahakikisha anapambana kwa lengo la kuhakikisha anaendelea pia kuaminika na benchi la ufundi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Joshua alisema licha ya ofa nyingi alizokuwa nazo ila amefikia uamuzi wa kujiunga na Fountain Gate, baada ya kuridhika na kile alichokihitaji, ikiwemo suala nzima la masilahi yake binafsi aliyokuwa ameyaweka mezani.

“Kwa msimu uliopita Fountain ilikuwa katika hali ya presha ya kushuka daraja, hivyo tunahitaji kuondoa hilo lisijirudie tena, pia nahitaji kufunga zaidi mabao kwa sababu ndio kazi yangu iliyonileta hapa kama mshambuliaji,” alisema Joshua.

Kwa upande wa Kocha wa Fountain Gate, Denis Kitambi, alisema anaamini mshambuliaji huyo atafanya vizuri na kikosi hicho kutokana na ubora wake aliouonyesha msimu uliopita akiwa na KenGold na baadaye kujiunga na ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo.

Nyota huyo amejiunga na Fountain Gate baada ya kuondoka Namungo aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025, akitokea KenGold ya jijini Mbeya ambayo imeshuka daraja kwa msimu wa 2024-2025, ikitokea Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship.

Joshua alijiunga na KenGold Agosti 2024, akitokea Tusker FC ya Kenya ambapo hadi anaondoka dirisha dogo, aliifungia timu hiyo mabao manne ya Ligi Kuu, huku kwa upande wa Namungo aliyoichezea kwa miezi sita akikifungia kikosi hicho bao moja.