Dk Mwinyi aeleza atakavyofungua Pemba

Unguja. Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amesema Pemba inafunguka kupitia bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao mwezi huu wanamkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi.

Pamoja na miradi hiyo, Dk Mwinyi amesema neema inakwenda kuwashukia wakulima wa karafuu na mwani, kwani tayari Serikali inayoongozwa na CCM imeshaweka mikakati mikubwa ya kuinua mazao hayo, yatakayokuza uchumi wa wananchi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, wakati akizindua kampeni za chama hicho kwa Upande wa Pemba katika viwanja vya Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba.


“Ndugu zangu, hakuna sababu kwa nini Pemba isifunguke. Septemba 25 tunamkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba. Pia kuna bandari zilizojengwa na zinaendelea kujengwa. Pemba itafunguka,” amesema Dk Mwinyi.

Mbali na uwanja wa ndege, amesema pia mkandarasi huyo atakabidhiwa ujenzi wa barabara ya Chakechake, mkoani Pemba, itakayokuwa kiunganishi cha usafirishaji kutoka bandari ya mkoani kwenda maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho.

Amesema bandari za Mkoani na Shumba zinakwenda kubadilisha uchumi wa Pemba, kwani meli kubwa za kimataifa zitakuwa zinashusha mizigo yake moja kwa moja katika bandari hizo.

Akizungumza kuhusu karafuu, Dk Mwinyi amesema, licha ya zao hilo kuwa zao kuu la biashara kisiwani humo, wananchi walikuwa wamekataa tamaa na kuyatelekeza mashamba.

Hata hivyo, amewataka wakulima waanze kuyafufua mashamba yao, akisema neema inakuja kwani wanakwenda kuliweka mazingira mazuri.

“Zao letu la karafuu limekuwa likipata changamoto, na imefika hatua wakulima wakayatelekeza mashamba. Sasa nawaambia kila mwenye shamba lake alishikilie, tuyatunze, neema inakuja,” amesema.

Mgombea urais wa CCM Dk Hussein Mwinyi akionyesha kadi za wanachama wa ACT Wazalendo aliowapokea leo na kuhamia chama hicho kisiwani Pemba



Kuhusu mwani, Dk Mwinyi amesema wanakwenda kuongeza vifaa kwa wakulima na tayari wamejenga kiwanda cha Manangwe, kitakachotumika kuchakata zao hilo.

“Tutaendelea kuwapa vifaa vya kisasa, tutanunua zao hilo kuchakata kiwandani, hivyo hakutakuwa na tatizo tena la soko. Haya ndio tunakwenda kuyamalizia,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema katika awamu ijayo, iwapo wakipewa ridhaa, wanataka kuleta mabadiliko makubwa hususani katika kisiwa hicho.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kuichagua chama hicho ili wakamilishe mambo mazuri waliyoyaanza, huku akitupa donge kwa wapinzani wake kwamba hawana sera.

“Msidanganywe na chochote. Kwanza, hao hawana sera. Haya tuliyoyasema hapa mmeshasikia wanayasema,” amehoji huku wananchi wakimjibu kwa kusema hapana.

Awali, akimkaribisha Dk Mwinyi na kumwombea kura, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose Migiro, amesema Serikali ya awamu ya nane inastahili kuungwa mkono kwa sababu imefanya mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanyika.