Arusha. Mahakama Kuu Masilaja Ndogo ya Tanga imemuachia huru Hussein Athumani, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mdogo wake.
Hussein alishtakiwa kwa kosa la ubakaji aliolidaiwa kutendwa mara mbili katika eneo la Amboni, mkoani Tanga.
Jaji Happiness Ndesamburo, aliyesikiliza rufaa hiyo iliyokuwa imekatwa na Hussein, alitoa hukumu hiyo Septemba 11, 2025, na nakala ya hukumu hiyo imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Amesema baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa, Mahakama hiyo imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo.
Hussein alishtakiwa kumbaka mdogo wake aliyekuwa na umri wa miaka 14, na upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano.
Madai yaliashiria kuwa kabla ya tukio hilo, shahidi wa pili (baba wa mwathirika) aliishi na Amina Omary (mama wa mrufani) kama wake na mume.
Mrufani ambaye alikuwa mtoto wa kuzaliwa wa Amina, mwathirika wa tukio hilo alikuwa binti wa shahidi wa pili (aliyempata katika ndoa ya awali) kabla ya kumuoa Amina.
Wawili hao (Amina na shahidi wa pili wa Jamhuri), walikubaliana mrufani aliyekuwa akiishi Kondoa, aende akaishi nao mkoani Tanga walipokuwa wakiishi wao na mwathirika wa tukio hilo, binti wa Amina (Maria).
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri (mwathirika) alidai Mei 4, 2022, mrufani alingia chumbani kwake bila kibali, akamfunika mdomo na kumbaka, jambo lililosababisha maumivu na kutokwa na damu.
Alidai wazazi wake waliporejea siku iliyofuata, alimweleza Amina (mama wa kambo) ambaye alikataa madai hayo na kumtishia kumfanyia vurugu iwapo atamwambia baba yake.
Tukio la pili lilidaiwa kutokea Novemba 19, 2023, mrufani alimbaka tena wakati (Amina) akiwa sebuleni na kuwa licha ya kupiga kelele kuomba msaada alipuuzwa na kuwa siku iliyofuata alifichua tukio hilo kwa dada yake (shahidi wa nne) ambaye alimjulisha baba yao.
Alidai kuwa baba yao (shahidi wa pili) alimuuliza kuhusu tukio hilo na kuwa alimweleza aliogopa kusema, ambapo alipelekwa kituo cha polisi, kisha hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Shahidi wa tatu, Mganga Msaidizi wa hospitali ya Ngamiani, Salehe Mayanju alithibitisha kumfanyia uchunguzi wa kimwili shahidi huyo wa kwanza alibaini kutokuwepo kwa michubuko ila kitu butu kilikuwa kimepenya.
Shahidi wa kwanza wa utetezi (mrufani) alikanusha madai hayo, akieleza kuwa walikuwa wakiishi nyumba moja lakini ana chumba chake, ila ana chumba chake na kudai shahidi wa kwanza alihisiwa na mama yake (Amina) kuwa ni mjamzito hivyo akampeleka kumpima.
Alidai kuwa baada ya kugundulika kuwa mjamzito, baba yake (shahidi wa pili) alimpeleka kutoa mimba hiyo.
Alidai aliteswa na polisi wakati wa uchunguzi na kulazimishwa kukiri, jambo alilopinga, na baadaye aliachiwa kwa dhamana.
Shahidi wa pili wa upande wa utetezi (Amina) mama wa mrufani, aliieleza Mahakama kuwa alishuku mwathirika wa tukio hilo alikuwa mjamzito baada ya kuona mabadiliko ya tabia yake pamoja na kutapika.
Alidai kuwa alimuona shahidi wa pili, akitoka chumbani kwa mwathirika wa tukio hilo, jambo lililoibua shaka ya uhusiano usiofaa na kuwa baada ya binti huyo kuwa mjamzito, shahidi wa pili wa Jamhuri aliitoa.
Aidha, alikanusha mrufani kumbaka mwathirika wa tukio hilo na kuwa kwa wakati huo alikuwa amehama akiishi kwa kujitegemea.
Mrufani alikuwa na sababu nne ambazo ni alitiwa hatiani kwa ushahidi dhaifu, wenye shaka na usioaminika, hakimu alikosea kumtia hatiani huku akishindwa kuona kuwa kesi ilipikwa kutokana na mgogoro wa wazazi.
Sababu nyingine ni hakimu alikosea kisheria kwa kumtia hatiani huku akishindwa kuzingatia na kutathmini ushahidi wa utetezi na pia hakimu alikosea kisheria kwa kushindwa kutambua kwamba kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila shaka yoyote.
Katika rufaa hiyo mrufani alijiwakilisha mwenyewe bila kuwa na wakili huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na Wakili Eric Mosha, aliyepinga rufaa hiyo na kueleza upande wa mashtaka ulithibitisha kosa.
Jaji amesema baada ya kuchunguza sababu zote nne za rufaa, hoja ya msingi ni iwapo upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi ya mrufani bila kuacha shaka yoyote.
Amesema katika kesi za jinai ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka, na kuwa moja ya jukumu la mahakama hiyo ya kwanza ya rufaa ni kutathmini upya ushahidi wote.
Kuhusu mwathirika wa tukio hilo, kudai kubakwa mara mbili na mrufani, Jaji amesema kuwa Mahakama hiyo imepewa mamlaka ya kutathmini upya ushahidi uliotolewa na kuwa atautathmini upya ushahidi huyo ili kubaini kama yeye alikuwa, shahidi wa ukweli, kama mahakama ya kesi ilivyopata.
Amesema baada ya kutathmini upya ushahidi kwenye rekodi hiyo na kuwa madai ya mrufani kuwa kesi hiyo ilitokana na mgogoro uliokuwepo kati ya baba wa mwathirika wa tukio hilo na mama yake, anaona ingawa ushahidi wa upande wa utetezi haukuthibitishwa kivyake, ulitosha kuibua shaka.
Jaji Ndesamburo amesema ushahidi wa shahidi wa kwanza umejaa mashaka, hauna ukweli na kuhitimisha kwa kuhusu rufaa hiyo, kufuta hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani na kuamuru aachiliwe mara moja.