Katika lugha ya Kichaga, Majalio ni jina lenye tafsiri sawa na Majaliwa. Mtoto mwenye kuitwa hivyo hu-beba ishara ya matokeo makubwa kwenye ukuaji. Yanaweza kuwa maono, ubashiri au matamanio ya wazazi kuona mtoto wao anakuwa na hadhi kijamii, kwa hiyo wanamwita Majalio, yaani Majaliwa.
Mei 10, 1980, katika familia ya baba Paul Henry Kyara na mkewe Anitha, alipatikana mtoto. Mama mzazi wa Paul, Pelegia Kimatare Kyara, alimtazama mjukuu wake baada ya kuzaliwa, akasema: “Huyu ni Majalio. Namwona mjukuu wangu akiwa mtu mkubwa. Jina linalomfaa ni Majalio.” Jina lilipokelewa na likawa!
Majalio ndiye Majalio Paul Kyara, Katibu Mkuu wa chama cha Sauti ya Umma (SAU), vilevile mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu 2025. Majalio anaamini kuwa maono ya bibi yake yanaweza kutimia Oktoba 29, 2025 Watanzania wakimchagua kwa kura nyingi ili aongoze dola ya Tanzania.
Paul Kyara, kama jina la kati na ukoo kutoka kwa Majalio, linawakilisha utambulisho wa mwanasiasa mwandamizi Tanzania, mwanachama wa mwanzo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vilevile mwasisi na kiongozi wa SAU. Majalio ni mtoto wa kwanza kati ya sita wa Paul Kyara na Anitha.
Anasema kuwa pamoja na maono ya bibi yake kwake, yeye mwenyewe katika ukuaji wake amekuwa akitokewa na ndoto za mara kwa mara, zenye kumwonesha akikabidhiwa uongozi wa juu kabisa wa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaamini hizo si ndoto tupu, bali maono na inawezekana maono hayo yakatimia baada ya Oktoba 29, 2025.
Mwaka 1999, Majalio alipokuwa na umri wa miaka 19, alianza safari ya kuyaelekea maono. Alijiunga na Chadema akiwa mwanachama wa kawaida, kijana, na akawa anashiriki harakati za kujenga chama. Ni Chadema ile “Chadema Vema”, ambayo bendera yake ilikuwa na rangi moja tu, bluu bahari. Na kwa vile baba yake alikuwa mwanachama mwandamizi na kiongozi Chadema, aliona ndipo palipo na mlango sa-hihi wa maono.
Mwaka 2000, baada ya kuona ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania inamrudia mara kwa mara, alimshirikisha mama yake, Anitha Kyara. Hata hivyo, mama yake hakuona kama kuna tafsiri yoyote zaidi ya ndoto. Mama alicheka na hakutilia maanani. Majalio ndoto ziliendelea hata alipofikisha umri wa mi-aka 25.
Februari 17, 2005, SAU ilipata usajili wa kudumu. Ni chama kilichozaliwa baada ya wanachama waandamizi wa Chadema kujitenga na kusisi chama kipya. Erick Mchatta alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa SAU, Paul Kyara- Katibu Mkuu. Majalio naye alijiunga na SAU.
Chanzo cha wana-Chadema waandamizi, wakiongozwa na Kyara kujitenga, ni uchaguzi mkuu Chadema uliofanyika PTA Sabasaba, Temeke, Dar es Salaam, mwaka 2004. Kyara alidai kushinda nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, lakini uchaguzi ukalazimishwa kurejewa mara mbili kwa sababu kuna viongozi hawakumta-ka, ila walimtaka wao.
Baada ya kujiunga SAU, Majalio alikuwa mwanachama wa kawaida mpaka mwaka 2008, alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Pwani. Aliishikilia nafasi hiyo kwa miaka tisa. Mwaka 2017, aliteuliwa kuingia katika sekretarieti akiwa Mkurugenzi wa Fedha, kisha mwaka 2018 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu. Nafasi hiyo anaishikilia hadi sasa.
Maisha ya Majalio duniani yalianzia Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mei 10, 1980. Mwaka 1988 alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Ubungo National Housing. Alisoma shuleni hapo hadi darasa la pili kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Mapambano, alikomaliza darasa la saba mwaka 1994.
Mwaka 1995, Majalio alijiunga na Sekondari Jitegemee, Temeke, Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1998. Mwaka 1999 akajiunga na Chuo cha Magogoni, alikosomea Utalii na kupata astasha-hada. Mwaka 2000–2002, alisoma ngazi ya diploma masomo ya Uhasibu na Uongozi wa Hoteli katika Chuo cha Masoka, Kilimanjaro. Hivi sasa, Taasisi ya Masoka ni kitivo cha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi.
Katika mahafali ya Chuo cha Masoka mwaka 2002, mgeni rasmi alikuwa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa (aliyekuwa madarakani). Majalio, mbali na kukabidhiwa cheti chake cha diploma ya Uhasibu na Uongozi wa Hoteli, pia alitunukiwa cheti cha mwanafunzi bora wa jumla alichopewa na Rais Mkapa.
Baada ya kumaliza masomo hayo ya diploma, alijikita kwenye biashara na kilimo, ingawa hakuacha kujiendeleza kwa kozi mbalimbali, ambazo alisoma kupitia mtandao. Moja ya kozi hizo ni Usimamizi wa Biashara, iliyomchukua miezi sita kuikamilisha kupitia Chuo cha Abu, kilichopo Malaysia. Kingine, Majalio amesomea masoko na usanifu katika kozi fupi.
Majalio ni mmiliki na kiongozi wa maduka ya dawa za binadamu ya MK Pharmacies, Hoteli ya Legho, Ubungo, Dar es Salaam. Anamiliki kampuni ya kutoa huduma za kuua wadudu, vilevile ni mkulima wa mahindi ambaye mashamba yake yapo Kibaigwa, Dodoma.
Mwaka 2005, Majalio alipokuwa na umri wa miaka 25, alijitokeza kuwania jimbo la Kibiti, Pwani. Mwaka 2010, aliingia ulingoni jimbo la Kibaha Mjini. Alirejea tena Kibaha Mjini mwaka 2020. Mara zote hizo aliwania ubunge kwa tiketi ya SAU, lakini hakufanikiwa.
Kumbukumbu hizo ni kuonesha kwamba Majalio amekuwa kwenye siasa za ushindani kwa miongo miwili. Ndani ya kipindi hicho, Tanzania imefanya Uchaguzi Mkuu mara nne na Oktoba 29, 2025, utafan-yika wa tano. Mara hizo tano, Majalio ameshiriki moja kwa moja majaribio manne; ubunge mara tatu na urais mara moja. Ni Uchaguzi Mkuu wa 2015 pekee ndiyo Majalio hakushiriki.
Majalio anasema akichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atawajenga wananchi, hasa watumishi wa umma, wawe na hofu ya Mungu. Anaamini kuwa taifa likiwa na watu wenye hofu ya Mungu, amani, upendo na uadilifu vitashamiri.
Anasema ukosefu wa maadili kwenye siasa na utumishi wa umma, chanzo chake ni watu kukosa hofu ya Mungu. Anataka kulishughulikia hilo kwa nafasi ya kwanza akiwa Rais.
Majalio anasema kuwa Serikali ya SAU, ambayo yeye ataiongoza, itajikita kwenye mambo matatu am-bayo ni kilimo, viwanda na teknolojia. Anafafanua kuwa utafiti waluoufanya umewapa majibu kwamba tatizo kubwa la ajira Tanzania litapata utatuzi endapo mambo hayo matatu yatashughulikiwa kwa pamoja.
Ahadi ya Majalio, kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya SAU, ni kwamba ndani ya miaka mi-tano, kupitia nguvu kubwa watakayoiweka kwenye kilimo, viwanda na teknolojia, wanatarajia kuten-geneza ajira milioni 10.
Kilimo Uhai ni programu ambayo Sau wanaahidi kuja nayo, kwa kuhakikisha kunakuwa na matumizi ya mbegu za asili, vilevile kilimo cha kisasa bila kemikali.
Mkazo wake kwenye mifugo ni kuwa machinjio yatakuwepo vijijini. Mijini na nje ya nchi zitasafirishwa nyama. Anatoa mfano kuwa kutoa ng’ombe Shinyanga kumsafirisha hadi Dar es Salaam kuchinjwa ni makosa kwa sababu Dar hakuna malisho bora. Ubora wa nyama unapungua njiani kwa kutandikwa, pia ukosefu wa chakula husababisha ng’ombe wale mchanga Dar.
Majalio anasema ngozi pia ubora wake hupungua kwa sababu njiani wanyama wanachapwa bakora. Kingine, ng’ombe huweza kupata magonjwa, matokeo yake ngozi hupungua ubora. Anaeleza kuwa kitendo cha wanyama kuchinjwa vijijini kitasaidia kupatikana nyama bora, pia ngozi safi.
Akichambua zaidi, Majalio anasema mabaki ya ng’ombe Dar es Salaam yanatupwa na kusababisha uchafu pamoja na uharibifu wa mazingira. Wakati vijijini, yangetumika kama mbolea. Anatoa mfano wa hali ya hewa ilivyo mbaya Soko la Shekilango, Ubungo, kwa sababu kuku huchinjwa sokoni hapo. Anaamini kwamba kuku wangechinjwa vijijini kungeepusha uchafuzi huo wa hali ya hewa, lakini pia mabaki hayo ya kuku yangekuwa mbolea vijijini.
Matilda Majalio Kyara ni mke wa Majalio. Katika ndoa yao, walifanikiwa kupata watoto sita, waliopo hai ni wanne. Mwanaye wa kwanza ni Michelle. Uzao wa pili uliwapa mapacha watatu— Milka, Milcent na Marlyn ambao walizaliwa kabla ya wakati (njiti).
Majalio anasema, kutokana na uwezo mdogo wa kitabibu na ukosefu wa vifaa bora vya kukuzia watoto waliozaliwa kabla ya wakati, Milka alifariki dunia ndani ya saa 24. Milcent alipoteza maisha baada ya siku 10. Marlyn ndiye alipona, baada ya kuwahishwa Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, Kenya. Watoto ni Melvin na Millan.
Majalio anashukuru kwamba familia yake inamuunga mkono kwenye harakati zake za kisiasa. Siku ya uzinduzi wa kampeni zake za urais, zilizofanyika Septemba 6, 2025, Ukonga, Dar, mama mzazi wa Majalio na mke wake, walikuwepo.