Mwanza. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kuwa, kikichaguliwa kuunda Serikali baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, kitahakikisha Jimbo la Buchosa linaunganishwa kwa barabara ya lami na Wilaya ya Sengerema pamoja na Mkoa wa Geita.
Kwa sasa, wananchi wa Buchosa wanalalamikia ubovu wa miundombinu kutoka Nyehunge kwenda wilayani Sengerema, hali inayosababisha usafiri kuwa wa gharama kubwa. Nauli ya kwenda na kurudi kutoka Nyehunge hadi Sengerema ni Sh6,000 msimu wa kiangazi na kufikia Sh8,000 msimu wa masika.
Mzee Joseph Mayeka, mkazi wa Buchosa, amesema ugumu wa maisha unachangiwa na hali ya ubovu wa barabara.
“Watoto wetu hata hawajui barabara ya lami inaonekanaje. Tuliahidiwa barabara mwanzoni mwa mwaka jana, lakini wakandarasi waliondoka kimya kimya na hatujui sababu,” amesema.
Mayeka ameongeza kuwa barabara ikijengwa, nauli inaweza kushuka hadi Sh700, hivyo kupunguza gharama za maisha kwa kiwango kikubwa.
Ahadi hiyo ya Chaumma imetolewa na mgombea urais wake, Salum Mwalimu, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukokwa, jimbo la Buchosa, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Jumatatu, Septemba 15, 2025, akiwa njiani kwenda Nyehunge kufanya mkutano wa hadhara wa kunadi sera.

Mwalimu amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utawala wake, barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami ili kupunguza gharama za usafiri na maisha kwa ujumla, na kuchochea maendeleo.
“Tutaiunganisha Buchosa na Sengerema kwa barabara ya lami. Nendeni mkachague upinzani, muone kama barabara haitajengwa. Acheni kuikumbatia CCM, ambayo imeshindwa kutimiza ahadi hiyo kwa miaka mingi,” amesema Mwalimu.
Kwa mujibu wa Mwalimu, akipatiwa ridhaa amedhamiria kuwatumikia Watanzania, na hata baraza la mawaziri atakaloliunda litakuwa na vijana wengi watakaomsaidia kusukuma mbele maendeleo.
Kwa upande mwingine, Mwalimu amewataka vijana waache kuwekeza nguvu kwenye kamari, na badala yake wamchague ili awape ajira kupitia uwekezaji wa rasilimali zilizopo.
“Nipo tayari kuwajibika mbele yenu miaka mitano ijayo. Mkiamua kunihukumu, hata kuandamana kuniondoa Ikulu mtakuwa na haki hiyo,” amesema kwa msisitizo.
Naye John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chaumma, ameeleza kuwa Buchosa imetelekezwa kwa sababu ya uaminifu wake kwa chama tawala (CCM), hali iliyosababisha kupitwa na maendeleo.
“Hamna hata kipande cha barabara ya lami. Mkiendelea kuwa wategemezi wa CCM, mtakosa maendeleo, mpeni kura za ndiyo mgombea urais wa Chaumma amalize matatizo yote haya,” amesema Mrema.

Naye Esther Fulano, mgombea ubunge Buchosa kupitia Chaumma, amesema dhamira yake ni kupigania huduma bora kwa wananchi.
Ameahidi kuwa, endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, kipaumbele chake cha kwanza ni kushughulikia changamoto za elimu, maji, afya na uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Buchosa tuna misitu ya mbao, lakini watoto wetu hawana madawati. Tukichaguliwa, tutasimamia rasilimali hizi ziwanufaishe wananchi,” amesema Fulano.