Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amerusha karata nyingine katika harakati za kujiondoa kwenye kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya kupinga hati ya shtaka linalomkabili akidai ni batili kutokana na kukiuka masharti ya sheria.
Hiyo ni hatua ya pili ya Lissu kutupa karata yake katika harakati za kujinasua na kesi hiyo baada ya kukwama hatua ya kwanza, alipopinga Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kuendelea kusikiliza kesi hiyo, akidai haina mamlaka hayo.
Hata hivyo, kabla ya kesi hiyo kuanza, Mwananchi ilishuhudia mvutano uliokuwa ukiendelea baina ya askari wa Jeshi la Polisi na baadhi ya wafuasi wa Chadema waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo.

Katika mvutano huo, askari takriban 30 waliokuwa wakilinda usalama katika viunga vya Mahakama, walishuhudiwa wakiwapiga baadhi ya wafuasi waliofika mahakamani hapo.
Mvutano huo ulitokana na wafuasi wa Chadema kutaka kuingia mahakamani, lakini polisi waliwaambia ukumbi umejaa na kuwataka waondoke.
Hata hivyo, wanachama hao walisisitiza kuwa nafasi ndani ya Mahakama bado ipo na wakaendelea kushinikiza waruhusiwe kuingia.
Baada ya sintofahamu hiyo ya mabishano, polisi walitoa amri ya kuwataka waondoke mara kadhaa wakisisitiza kuwa, ndani hakuna nafasi.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kukaidi amri hiyo, ndipo mmoja wa askari aliyedhaniwa kuwa kiongozi wa kikosi hicho alipotoa amri ya kuwatimua.

Baada ya amri hiyo, mvutano ulianza huku polisi wakitumia virungu dhidi ya wote walioonekana kukaidi agizo hilo, wengine wakikimbia huku baadhi yao wakikamatwa.
Purukushani hiyo ilidumu kwa takribani dakika nne hadi tano, hatua iliyomlazimu askari mmoja wa usalama barabarani (trafiki) aliyekuwapo eneo hilo, kuamuru magari kusimama, kwa muda usiopungua dakika mbili.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyodaiwa kutamka kuhusu kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.
Hata hivyo, Lissu aliibua pingamizi akiomba Mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iitupilie mbali akitoa sababu mbili, ubatili wa hati ya mashtaka na mamlaka ya Mahakama, ambayo leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, imekataa.
Baada ya Mahakama kukataa sababu hiyo ndipo Lissu akaendelea na sababu ya pili ya pingamizi lake, yaani ubatili wa hati ya mashtaka.
Madai ya ubatili wa hati ya mashtaka
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Lissu kabla ya kukubali au kukana, aliielekeza Mahakama kwenye vifungu vya 294 (1) na 295(1) vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marekebisho ya mwaka 2023.

Amedai kwa mujibu wa vifungu hivyo, hawezi kujibu shtaka hilo kwa sababu ana pingamizi dhidi ya uhalali wa hati ya mashtaka, mpaka litakapoamuliwa.
Lissu amedai hati hiyo haioneshi kosa lolote hasa la uhaini.
Amedai kuwa, msingi wa pingamizi lake uko katika kifungu cha 135 cha CPA, kinachoeleza kila hati ya mashtaka inapaswa kuwa na maelezo ya kosa analoshtakiwa nalo mshtakiwa na taarifa za msingi zinazotosheleza kuonesha asili ya kosa analotuhumiwa.
Amedai kuwa, hati ya mashtaka isipokuwa na taarifa hizo ni batili kwa mujibu wa Sheria za Tanzania.
Akizungumzia hati ya mashtaka ya kesi yake, Lissu amedai hati aliyosomewa alipopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu na aliyopewa Agosti 18, 2025, kesi hiyo ilipohamishiwa Mahakama Kuu, zinatofautiana.
Hata hivyo, amedai kwenye hati za mashtaka zote hakuna kosa la uhaini wala jinai kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na kwamba, ziko kinyume na masharti ya kifungu cha 135 cha CPA.
Akifafanua kasoro za hati hiyo ya mashtaka, Lissu amerejea Kifungu cha 39(2) (d) cha PC anachoshtakiwa nacho, kinachoeleza kuwa: (2) Mtu yeyote ambaye, yumo ndani ya Jamhuri ya Muungano, akiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano au popote, anajenga nia kusababisha au kuwezesha kusababishwa au anajenga nia ya kuchochea, anashawishi, anashauri au kuusia mtu yeyote au kikundi cha watu kusababisha au kuwezesha kusababishwa kati ya matendo au malengo yafuatayo, yaani:-
(d) Kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge na Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na kubainisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi au machapisho au kwa kitendo chochote cha siri kinachojionesha cha hali yoyote, atakuwa na hatia ya kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifo.”
Lissu amedai kuwa, kesi yake hiyo si ya kwanza ya uhaini nchini, bali ni ya tatu na hivyo, kuna mwongozo wa namna ya kuendesha shtaka la uhaini.
Amedai kuwa, kesi ya kwanza ni Grey Likungu Mattaka na wenzake akiwamo Bibi Titi Mohamed dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1970 katika Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki.
Amedai kuwa, kwa mujibu wa kesi hiyo lazima mshtakiwa awe na utii kwa Jamhuri, mbili lazima kuwe na nia ya kufanya uhaini na tatu nia hiyo lazima ionekane kwa maandishi au kwa matendo.
Amedai kuwa, kesi ya pili ilikuwa mwaka 1983 iliyomhusu Hatibu Gandhi na wenzake dhidi ya Jamhuri.
Akirejea hati ya shtaka la kesi yake, Lissu amedai kuwa, maelezo yanaeleza kuwa siku hiyo alitengeneza nia ya kuushawishi umma kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 usifanyike.
Amedai, kuwa katika kifungu hicho anachoshtakiwa nacho kina makosa 10 ya uhaini, lakini kuzuia uchaguzi mkuu si mojawapo ya makosa hayo na kwamba, hilo haliwezi kuwa uhaini wala kosa la jinai yoyote katika Sheria za Tanzania.

Akirejea Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Sura ya 7 ya mwaka 2024, alisema inatengeneza makosa 20 ya uchaguzi lakini hakuna hata moja la kuzuia uchaguzi.
Lissu amedai kuwa, nia ya uhaini lazima ionekane kwa kuchapisha au kwa matendo na kwamba, katika kesi yake maelezo ya kosa yanaeleza kuwa, alionesha nia ya uhaini kwa kutamka, huku akidai kuwa maneno matupu kwa mujibu wa kesi ya Hatibu Gandhi, hayatengenezi uhaini isipokuwa kama yanaelezea uhaini.
Pia, amedai kuwa kwa mujibu wa kesi hiyo maneno ya mtu mmoja hayawezi yakawa uhaini, huku akirejea neno moja moja kati ya maneno anayodaiwa kuyatamka na kutoa maana yake kwa mujibu wa Kamusi.
Amehoji ni wapi kuna uhaini katika maneno hayo huku akidai kuwa, hakuna mahali ambako ameitaja Serikali na vyombo vyake, Bunge, Mahakama wala viongozi wake.
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesi Jumanne, Septemba 16, 2025, ambapo Lissu ataendelea kuwasilisha hoja zake.