Mbarali. Mgombea Ubunge jimbo la Mbarali Mkoa wa Mbeya, Bahati Ndingo amesema endapo atapata ridhaa atahakikisha wakulima wanaondokana na kilimo cha kutegemea maji ya mito na mvua na baada ya Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa saba ya umwagiliaji.
Ndingo ametoa kauli hiyo leo Septemba 15, 2025 wakati wa kuomba kura kwa wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mswiswi wilayani humo.
Kampeni hiyo imezinduliwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea ubunge jimbo la Makambako Mkoa wa Njombe, Daniel Chongolo.
Ndingo amesema Wilaya ya Mbarali ni moja ya Wilaya nchini kinara kwa kuzalisha zao la mpunga na kwamba ujio wa kilimo cha umwagiliaji, kitaleta tija kubwa katika uzalishaji na kuinua uchumi wa wakulima.
“Tunatarajia wananchi wanakwenda kuondokana na changamoto ya kutegemea maji ya mvua na mito kwa ajili ya kumwagilia, lakini kwenye Ilani ya uchaguzi mwaka 2025/2030 Serikali inakuja na mpango wa ujenzi wa mabwawa saba ya kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Amesema uwepo wa kilimo cha umwagiliaji utaondoa changamoto kwa wakulima kutegemea msimu wa mvua pekee, niombe wananchi kujitokeza kupiga kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025,” amesema.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imejidhatiti kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi hususani uwekezaji katika sekta ya kilimo cha kisasa.
Naye Mratibu wa Kampeni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Daniel Chongolo amesema ni wakati wa kufanya maendeleo na kuachana na mazoea huku wakijitokeza kupiga kura kuchagua viongozi.
“Wana Mbarali ifikapo Oktoba 29, 2025 jitokezeni kwa wingi kupiga kura mafiga matatu za Rais, wabunge na madiwani ili maendeleo yawafikie kwa wakati husika,” amesema.
Naye mgombea udiwani Kata ya Rujewa, Jeremiah Makao amesema wananchi wana wajibu wa kupiga kura za kishindo kuchagua viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Wananchi wana matumaini sana na CCM kwa sababu ni mashuhuda wa miradi mingi ambayo imeletwa na Serikali ya awamu ya sita,”amesema.
Wakizungumza na Mwananchi Digital wananchi wa Kata ya Kongoro Mswiswi, Ebron Amon amesema hatua ya Serikali kuja na mpango wa ujenzi wa mabwani ni suluhisho kubwa la kuondoa changamoto katika sekta ya kilimo.
Kuna kipindi mvua zinakuwa za shida mazao yanakauka na kusababisha kukwama kurejesha mikopo ya pembejeo za kilimo kwa wakati,” amesema.