Njombe. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Bara, Stephen Wasira amesema miradi ya ujenzi na ufufuaji wa reli ikiwamo ya Tazara na ya kusini kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, italeta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini huku wakulima wakitarajiwa kunufaika kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 15, 2025 na viongozi wa CCM kutoka kata 37 za majimbo matatu ya Wilaya ya Njombe, Wasira ameeleza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030, ambayo inalenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuinua sekta ya kilimo.
“Kwa miaka mitano ijayo, Rais Samia Suluhu Hassan amesaini mkataba na Zambia pamoja na China kwa ajili ya kufufua reli ya Tazara inayopita Makambako. Reli hiyo itaunganisha maeneo haya na Uwanja wa Ndege wa Songwe pamoja na Bandari ya Dar es Salaam.

“Hii ilikuwa dhamira ya Mwalimu Nyerere tangu awali kuhakikisha mazao ya wakulima yanafika sokoni kwa urahisi kupitia reli,” amesema Wasira.
Pia, amebainisha kuwa ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kuiunganisha na maeneo ya Ludewa, utarahisisha usafirishaji wa rasilimali kama chuma cha Liganga na makaa ya mawe ya Nchuchuma.
Amesisitiza kuwa reli ndiyo suluhisho pekee kwa bidhaa hizo nzito.
“Serikali ya CCM inayokuja kwa miaka mitano ijayo italeta mabadiliko makubwa kwa maisha ya wakulima. Miundombinu hii itawawezesha kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi zaidi, jambo ambalo litakuza kipato chao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa maeneo haya,” amesema.
Wasira pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Njombe kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 29, 2025.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Makambako CCM, Daniel Chongolo ametoa wito kwa makada wa chama hicho kuendeleza mshikamano na ushirikiano ili kuhakikisha ushindi wa chama katika nafasi zote za uongozi.
Chongolo amesema mshikamano miongoni mwa makada ni silaha muhimu katika kutimiza malengo ya chama, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Tukisimama pamoja kama familia moja ya CCM, hakuna linalotushinda. Ushirikiano wetu ndiyo msingi wa ushindi wetu,” amesema Chongolo.