Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeeleza kuwa askari wake walilazimika kujihami leo Septemba 15, 2025 baada ya kuzuka vurugu katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 15, 2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema vurugu hizo zilianza baada ya ukumbi uliokuwa ukitumika kwa ajili ya kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kujaa na kulazimika wafuasi wengine kukaa nje.
“Kulijitokeza kundi la wanachama wa Chadema ambao walikuwa nje ya Mahakama. Baadhi yao walianza fujo na kujaribu kuwashambulia askari waliokuwa wanalinda eneo hilo,” amesema Muliro.
Amesema kutokana na hali hiyo, askari walijibu kwa kujihami na kufanikiwa kutuliza vurugu hizo kwa haraka bila madhara makubwa kuripotiwa.
Hata hivyo, Muliro hakufafanua iwapo kuna watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo, zaidi akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitaruhusu vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali katika maeneo ya Mahakama.