Mwenyekiti marefarii wa Taekwondo duniani aipa neno Tanzania

Mwenyekiti wa marefari wa Shirikisho la Taekwondo la Dunia,  Dk Jun Cheol Yoon amesema Tanzania ina fursa ya kufanya vizuri kimataifa katika mchezo huo endapo itaongeza  nguvu kuandaa timu za vijana.

Yoon yupo nchini kuendesha mafunzo ya kimataifa ya makocha wa Taekwondo, yanayofanyika kwa wiki mbili hadi Septemba 26, 2025 kwenye Kituo cha Olympafrica kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Yoon amesema timu za vijana ndio msingi madhubuti katika michezo, akigusia pia falsafa ya Taekwondo aliyohitaji kuwa ni kutokata tamaa na kufanya kazi kwa ushirikiano.

“Mkiiheshimu hiyo falsafa mtafika levo ya juu, ili kufanikiwa inategemea ufundi ulioupata, nidhamu na moyo wa uvumilivu, mafunzo ni magumu, ukiachana na yale ya nadharia na ya vitendo ambayo tutayafanya, vilevile ili uwe mkakamavu, lazima upige push up 1000 na kuiweka misuli imara, yote yanategemea uwezo wenu kama mkiweka bidii katika elimu mnayopata, mtafika mbali na kutengeneza vijana ambao watakuwa na msaada katika timu za taifa lenu,” amesema Dk Yoon.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) yanadhaminiwa na Kituo cha Misaada cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) cha Olympic Solidarity (OS), yakiendeshwa na mkufunzi  huyo wa Shirikisho la Taekwondo la Dunia.

Rais wa TOC, Gulam Rashid amesema hayo ni mafunzo ya pili ya Taekwondo kuendeshwa na Kamati hiyo chini ya ufadhili wa OS.

“TOC kila mwaka tuna kozi mbili, hata hivyo tuna vyama 19, hivyo ukigawa mara mbili utaona  kila baada ya miaka tisa au zaidi ndipo chama kingine kinapata fursa hii.

“Ingependeza viongozi wetu wa vyama au mashirikisho ya michezo, wakati zamu yao haijafikiwa,  wakati mwingine wavitumie vyama vyao vya kimataifa kufanya kozi hizi,” amesema Gulam.

Taekwondo mara ya kwanza ilipata kozi hiyo mwaka 2014, iliyofanyika mjini Arusha na mwaka huu ni kozi ya pili ikishirikisha makocha 30 kutoka visiwa vya Unguja na Pemba, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam.

Katika mafunzo hayo, Gulam aliwasisitiza washiriki kuendeleza timu za vijana mara watakapohitimu ili ziwe chachu ya mafanikio kwenye timu za taifa za mchezo huo.

“Makocha wengi huwa tunasahau kwamba michezo inaanza na vijana, mfano katika mashindano ya Anoca (Nchi za Afrika Mwanachama wa Olimpiki) au kwenye michezo ya Olimpiki na Madola yapo mashindano ya vijana.

“Hiyo ni fursa nasi tuanze kuwafundisha vijana ili washiriki hayo mashindano makubwa, wenzetu wa mpira wa miguu wanapiga hatua kwa sababu wao wana timu za rika mbalimbali kwa jinsia zote, Taekwondo nanyi mwende huko, sio kwenye mashindano ya kimataifa nchi inapeleka mchezaji mmoja au wawili hatuwatendei haki vijana wetu,” amesema

Rais wa Shirikisho la Taekwondo Tanzania (TTF), Ramoudh Ally amesema mbali na kufundisha timu za wakubwa, makocha watakaohitimu kwenye mafunzo hayo watatakiwa pia kujikita kukuza vipaji vya vijana na watoto kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa.

“Hii ni kozi kubwa ya kimataifa ambayo ipo kwenye data base ya Shirikisho letu la dunia, utaalamu ambao makocha wetu wanaupata si kwamba utawasaidia wao pekee,  bali wakiutumia vema unakwenda kusaidia hadi kwenye timu zetu za taifa,” amesema Ally.

Kiongozi huyo aliwasisitiza makocha hao kujituma na kutengeneza network nzuri na mkufunzi ambaye pia ni mwenyekiti wa marefarii wa Taekwondo duniani, ili kwa baada wasiishie kuwa makocha tu, wapige hatua nyingine zaidi kwenye urefarii.