Wagosi wa kaya wapo tayari Bara

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Ally Ameir amesema kikosi hicho kipo tayari kukabiliana na Tanzania Prisons katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kupigwa Septemba 17, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Pambano hilo la Wagosi wa Kaya waliowahi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu (enzi za Ligi Daraja la Kwanza) mwaka 1988, ni kati ya mechi mbili zitakazofungua msimu mpya wa 2025-2026, mwingine ukiwa ni kati ya KMC dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo aliyetambulishwa hivi karibuni kutoka Zanzibar, alisema timu hiyo kimbinu, utimamu ipo tayari kuonyesha ushindani katika mechi hiyo ya kukata utepe wa msimu mpya, huku akiweka wazi kuwa amesuka kikosi bora cha ushindani.

“Tulikuwa na maandalizi mazuri kwa kucheza mechi nyingi za kirafiki na timu ambazo kwa asilimia kubwa tutakutana nazo msimu huu mikakati na mbinu mbalimbali nimezielekeza kwa wachezaji ambao wamenielewa,” alisema Kocha Ameir na kuongeza;

“Kilichobaki sasa ni kuimarisha ushindani kabla ya mechi hiyo ya kwanza wa msimu wa Ligi Kuu Bara tukianzia nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons, hatupo tayari kuanza vibaya nyumbani wana Tanga njooni kwa wingi kuipa sapoti timu ili kuongeza morali kwa wachezaji.”

Alisema ugeni wake katika timu hiyo umempa mwanya wa kufahamu ubora wa kila mchezaji kwani amekuwa akitoa mafunzo uwanja wa mazoezi kwa kutoa nafasi ya kila mchezaji kuonyesha alichonacho.

“Sina kikosi ya kwanza kila mchezaji ana nafasi ya kucheza kulingana na uwajibikaji wake kwenye uwanja wa mazoezi mechi za kirafiki tulizocheza zimenipa picha nzuri kutambua timu ina ubora kiasi gani na mapunguvu vitu ambavyo tayari nimevifanyia kazi,” alisema Ameir.

Kocha huyo juzi Jumapili aliiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APS Bomet katika mechi ya kirafiki maalumu iliyofungia tamasha la Wagosi lililotambulisha kikosi cha msimu  mpya wa 2025/26.