ALIYEKUWA kipa wa Dodoma Jiji, Mkongomani Alain Ngeleka, amesema Ligi Kuu Bara imempa fursa ya kuonekana zaidi baada ya nyota huyo kukamilisha uhamisho wa kujiunga na kikosi cha Bandari ya Kenya kwa ajili ya kukitumikia msimu wa 2025-2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngeleka alisema kucheza kwa muda mrefu katika Ligi Kuu Bara kumechangia kupata nafasi hiyo ya kujiunga na kikosi cha Bandari, hivyo atahakikisha anapambana pia zaidi na nyota wengine ili kuingia kikosi cha kwanza.
“Hii ni fursa nyingine ya kuendelea kukuza soka langu, nafurahia kwa nafasi niliyoipata Tanzania na sasa ni muda wangu wa kupata changamoto mpya, ninachoweza kujivunia ni ubora wa Ligi Kuu ambao umechangia hapa nilipo,” alisema Ngeleka.
Nyota huyo tayari ameichezea Bandari mechi moja ya kimataifa ya kirafiki, katika ‘Wiki ya Mwananchi’, Septemba 12, 2025, iliyoshuhudia kikosi hicho kutoka Kenya kikichapwa bao 1-0, dhidi ya Yanga lililofungwa na Celestin Ecua dakika ya pili.
Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu wa 2024-2025, akitokea Kagera Sugar, anakumbukwa msimu wa 2022-2023, akiwa na kikosi cha Tabora United zamani Kitayosce na alijiwekea rekodi nzuri ya kufunga bao katika Ligi ya Championship.
Ngeleka alifunga bao la kufutia machozi kwa upande wa Tabora United katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni na timu hiyo ilichapwa mabao 3-1, dhidi ya JKT Tanzania, Desemba 3, 2022.
Nyota huyo alijiunga na Tabora United wakati ikishiriki Championship kwa msimu wa 2022-2023, akitokea Klabu ya Lumwana Radiant ya Zambia, akizichezea pia Nkana na Buildcon za Zambia, Sanga Balende, Groupe Bazano na Tshinkunku FC za kwao DR Congo.