NIKAMJIBU: “RAISA, akijua, urafiki hautakuwepo tena kwa sababu nilimficha ukweli; na isitoshe, huyo Shefa alikuwa rafiki yake sana.”
“Sasa msubiri baba yako aje umueleze; usikie atakwambia nini.”
“Baba utamueleza wewe. Mimi siwezi kumueleza.”
“Basi msubiri. Aliniambia anakwenda benki. Pengine muda huu anarudi.”
Wakati mama ananiambia hivyo, Raisa akanipigia simu. Nikaipokea.
“Habari ya huko, shoga?” akanisalimia.
“Nzuri. Umeamkaje?”
“Nashukuru, kumekucha. Ndiyo, nakufuata — hivyo twende huko msibani.”
“Mimi sipo nyumbani, niko Sahare.”
“Jana si uliniambia kuwa leo twende tukampe pole mke wa Shefa?”
“Nilikwambia, lakini sikuamka vizuri. Najisikia kuumwa, ndiyo maana nimekuja kushinda huku.”
“Basi nitakwenda peke yangu. Nitakaporudi nitakupitia nyumbani kukujulia hali. Si utakuwa umesharudi?”
“Kwani utarudi saa ngapi?”
“Nitakaa mpaka mchana.”
“Nadhani utanikuta.”
“Basi ugua pole, tutaonana muda huo.”
“Sawa.”
Raisa akakata simu.
“Raisa huyo ananipigia simu, anataka twende tukampe pole mwenzetu,” nikamwambia mama.
“Unaweza kwenda hata kesho. Usipokwenda kabisa unaweza kueleweka vibaya.”
Ghafla baba akaingia.
“Shikamoo, baba,” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari yako?”
“Nzuri, baba. Unajionaje?”
“Nashukuru. Umekuja saa ngapi?”
“Kama saa moja hivi iliyopita.”
Baba akaingia chumbani. Mama niliyekuwa nimekaa naye alainuka na kumfuata. Nikajua amekwenda kumueleza zile habari.
Baada ya kama nusu saa hivi, mama na baba wakatoka; lakini baba alikuwa ametaharuki.
Baba alikaa kwenye kochi akaniuliza.
“Rukia, kuna habari gani?”
“Ni kama hivyo alivyokueleza mama.”
“Kwanini hukuja kutuambia mapema? Umekuwa na ujasiri gani wa kukaa na mwili wa mtu nyumbani kwako kwa siku mbili kisha kwenda kuutupa usiku?”
“Sasa ningefanyaje, baba, wakati balaa limeshanifika?”
“Yaani hapo, kwa vyovyote itakavyokuwa, muuaji utaonekana ni wewe. Huyo mwizi aliiba kitu hapo nyumbani?”
“Hakuna kitu chochote kilichoibiwa.”
“Sasa umejuaje kama alikuja mwizi?”
“Nimekisia tu kwa sababu dirisha lilivunjwa.”
“Inawezekana si mwizi, ni muuaji tu. Kama ni mwizi angeiba kitu. Mtu amekuja na rungu; utasema huyo ni mwizi kweli?”
“Sasa ni nani?”
“Unajua yule alikuwa mume wa mtu na wewe ni mke wa mtu, na alikuwa kwako usiku mwingi. Hilo kwanza ni kosa.”
“Hilo ni kosa, sawa. Lakini umesema aliyemuua Shefa si mwizi, atakuwa nani?”
“Inawezekana akawa mtu mwingine. Hilo linakuwa kama fumanizi.”
“Mume wangu alikuwa hayupo.”
“Na mke wa huyo rafiki wa mume wako alikuwa hayupo?”
“Yeye alikuwa nyumbani kwake.”
“Hapo watu wa kuwafikiria ni wengi. Inawezekana ni mume wako au mtu aliyetumwa na mke wa marehemu. Kwa sababu hilo ni fumanizi. Inaonekana huyo mtu aliuawa kwa ugomvi.”
“Yaani mke wake atume mtu amuue mume wake?”
“Inawezekana.”
“Akishamuua, iweje?”
“Akukomoe wewe.”
“Lakini sidhani; huyo mwanamke alikuwa anahangaika sana kumtafuta mume wake.”
“Binadamu ni wajanja sana, mwanangu.”
“Sijui.”
“Sisemi kama ni yeye moja kwa moja, ila anaweza pia kuwa mume wako. Pengine alikuja usiku akamuona, akamuua kwa kudhani ni mume mwenzake.”
“Mume wangu alikuwa safarini na ameniambia anarudi leo.”
“Anaweza kuwa amekudanganya. Si ajabu yuko hapa mjini. Labda aligundua kuwa ulikuwa na uhusiano na huyo rafiki yake.”
Nikajiuliza kimoyomoyo: Sufiani angejuaje kama nilikuwa na mpango wa kumuingiza Shefa mle ndani? Au Raisa aliamua kunigeuka akampigia simu mume wangu?
Maswali hayo yalikuwa yakipita kichwani mwangu bila kupata majibu.
Lakini kwa upande mwingine yalikuwa yamezindua kichwa changu kujua kuwa ule mpango wa mauaji ya Shefa unaweza pia kufanywa na mume wangu au mke wake Shefa.
Kitu cha msingi, nikajiambia, ni lazima nifanye uchunguzi ili kubaini kama kweli watu hao ndio waliohusika au ni shuku tu ya baba yangu.
Nikaendelea kujiambia kuwa, kama ni suala la kufanya uchunguzi, ni lazima niufanye haraka kabla sijakamatwa; kwani nitakapokuwa mikononi mwa polisi sitaweza tena kufanya uchunguzi huo.
“Hebu twende huko nyumbani kwako ukanionyeshe hilo tukio lilivyotokea,” baba akaniambia aliponiona nilikuwa kimya nikiwaza.
“Sawa, twende ukaone.”
“Utataka na wewe uende ukaone?” baba akamuuliza mama.
“Tunaweza tukaenda sote ili tushauriane.”
Baba akanitazama.
“Mbona sikuona gari yako hapo nje, hukuja nayo?” akaniuliza.
“Nimeiacha. Naogopa kutembea nayo,” nikamjibu.
Dakika chache baadaye tukawa kwenye teksi tukielekea nyumbani kwangu.
Tulipofika nyumbani tuliingia ndani. Nikawaonesha wazazi wangu dirisha lililovunjwa kisha nikawaonesha mahali nilipomkuta Shefa akiwa ameshauawa.
“Ulivyomuona, ulihisi alikuwa akitoka Maliwatoni au alikuwa akienda sasa?” baba akaniuliza.
“Nadhani alikuwa akitoka Maliwatoni.”
“Sio kwamba alikuwa akienda sasa; huyo mtu akampiga kwa nyuma?”
“Sasa hapo sina hakika.”
“Kwani alipigwa sehemu gani kichwani?”
“Alipigwa upande wa kushoto wa kichwa chake.”
“Karibu na kichogo au karibu na komo lake?”
“Karibu na kichogo.”
“Kama ni karibu na kichogo, ni lazima aliyempiga alimpiga kwa nyuma. Hiyo inaonyesha kuwa alipigwa wakati anakwenda sasa Maliwatoni. Aliyempiga alikuwa amemvizia na alikuwa na dhamiri ya kumuua. Siyo mwizi.”
Baba yangu aliwahi kuniambia kuwa aliwahi kufanya kazi ya upolisi na akawa mpelelezi kabla ya kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma za kupokea rushwa. Wakati huo mimi nilikuwa sijazaliwa.
Sasa, jinsi alivyokuwa akiyatafsiri yale matukio yalivyotokea kwa utaalamu, niliamini kuwa alikuwa mpelelezi hodari.
“Mimi naamini aliyemuua huyu kijana alikusudia kuja kumuua. Sasa swali la kujiuliza, huyu Shefa hakai hapa na alikuja hapa kwa siri usiku; huyo mtu alijuaje kama yuko hapa?” baba akatuuliza.
Hakukuwa na yeyote aliyemjibu. Baba alitutazama kwa zamu tukisubiri jibu. Alipoona tupo kimya akaendelea.
“Lazima ukubali kuwa mlikuwa mnafuatiliwa. Na haya mauaji ni ya fumanizi. Muuaji yuko pembeni na anakutazama unavyohangaika. Mwisho wa siku, unakamatwa wewe!” baba yangu, kachero wa zamani, akaniambia.
Maneno yake yaliniongezea hofu.
“Sasa, baba, nifanyeje?” nikamuuliza kwa sauti iliyoodhihirisha hofu yangu.
“Ulikosea tangu mwanzo. Usingemruhusu huyu mtu aje nyumbani wako wakati mume wako hayupo.”
“Sikumruhusu, baba. Alikuja mwenyewe. Hii nyumba ameizoea.”
“Alikuja mwenyewe saa sita usiku? Nani alimfungulia mlango?”
“Alibisha mlango nikamfungulia.”
“Kwanini ulimfungulia?”
“Sasa ningefanyaje, baba, wakati huyo mtu ni rafiki wa mume wangu na anakuja hapa nyumbani mara kwa mara?”
“Sasa hatari yake ndiyo hii. Hapa huwezi kupata ujanja wa kujinasua. Cha kuomba hapa, namba za gari lako zisitajwe na huyo bodaboda uliyesema alikuona ukitupa huo mwili akiwa pamoja na Raisa.”
“Yeye amenihakikishia kuwa hatataja kwa sababu hataki kujiingiza katika ushahidi. Na pia hakunibainishia wazi kama aliziona namba hizo au la.”
“Wakati anakwambia hivyo, alikuwa anajua kwamba uliyefanya kitendo hicho ni wewe?”
“Alikuwa hajui kama ni mimi.”
“Lile rungu nalo ulikwenda kulitupa?”
“Lipo.”
“Liko wapi?”
“Liko stoo. Kama unataka kuliona, njoo huku stoo nikuonyeshe.”
Nikaenda kwenye mlango wa stoo na kuufungua. Hatukuingia ndani. Tulisimama mbele ya mlango. Rungu hilo lilikuwa likionekana kwenye sakafu ya stoo.
“Ni lile pale,” nikamwambia.
Damu iliyokuwa imeingia kwenye rungu hilo ilikuwa imeganda na kuwa nyeusi.
“Na ile ni damu?” baba akaniuliza.
“Ile ni damu imeganda.”
“Lile rungu ulilishika kwa mikono yako?”
“Ndiyo, nililishika nikaliingiza huku stoo.”
Baba akatikisa kichwa kwa kusikitika.
“Binti yangu, unajiletea matatizo yasiyokuwa na sababu.”
“Sasa, baba, ningeliingizaje bila kulishika?”
“Kama umelishika, maana yake ni kwamba umeshafuta alama za vidole za muuaji na kuweka alama zako. Sasa rungu lile likipatikana na polisi na kuchunguzwa linaweza kukutwa na alama zako.”
“Si nitawaeleza ukweli kuwa nililishika?”
“Sasa watakuuliza ni kwanini hukutoa ripoti polisi; utajibu nini?”
Nikanyamza kimya. Baba akajibu mwenyewe swali lake: “Jibu watakuwa nalo polisi kwa sababu najua wewe hutajibu kitu.”
“Hao polisi watakuwa na jibu gani?” mama akamuuliza.
“Watakuwa na jibu kwamba Rukia hakutoa ripoti polisi kwa sababu ndiye aliyemuua marehemu!”
Sote tukabaki kutazamana kwa fadhaa.
“Liondoe lile rungu ulifiche pembeni,” baba akaniambia kwa ukali kidogo.
“Baba si umesema nisilishike?” nikamuuliza.
“Kama ni kulishika umeshalishika; sasa liondoe tu. Kama utalifunika kwa kitu kama tambara itakuwa vyema zaidi. Alama zako hazitatokea.”
“Itasaidia nini baba wakati nimeshalishika?”
“Hilo tambara litafuta alama zako kama bado zipo.”
“Labda nlioshe kabisa halafu usiku niende nikalitupe.”
“Basi fanya hivyo.”
“Nitasubiri usiku nitaliosha halafu nitaenda kulitupa mbali.”
“Na unapokwenda kulitupa pia lishike na kitu kingine; usisahau na kulishika kwa mkono wako.”
“Kwa vile umeshaniambia, sitasahau.”