Wananchi Watakiwa Kuzingatia Taratibu za Uchimbaji Visima, Wahimizwa Kutumia Maji ya Bomba

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imewataka wananchi kuzingatia taratibu za uchimbaji wa visima na kuendelea kutumia maji ya bomba ambayo yamehakikishwa usalama wake.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa usambazi wa maji safi na usafi wa mazingira kutoka SOUWASA Mhandisi Jafari Yahaya, amesema uchimbaji wa visima si kosa, lakini lazima ufanyike kwa kufuata taratibu, amesisitiza kuwa visima vyenye urefu unaozidi mita 15 vinapaswa kuchimbwa kwa kibali cha Mamlaka ya Bonde la Mto Ruvuma na Ziwa Nyasa, na kila kisima kiwe angalau mita 50 kutoka chooni ili kuzuia kuingia kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya mlipuko.

Ameeleza kuwa kwa sasa asilimia 94.3 ya wakazi wa Songea wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia mtandao wa SOUWASA, akigusia miaka kadhaa iliyopita kuna utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Hospitali ya Mkoa katika mtaa wa Merikebu Bombambili ulibaini madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya maji ya visima, ameeleza Kupitia elimu waliyoitoa kwa sasa wananchi wengi wameacha kutumia maji ya visima na kuhamia kwenye maji ya bomba.

Mhandisi Yahaya amewashauri wananchi kupima ubora wa maji yao katika maabara ya mkoa kwani ni  gharama nafuu huku akionya kuwa wale wanaochimba visima bila  vibali, endapo kutasababisha madhara, hatua za kisheria huchukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Stanley Mgeni, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, amesema kumekuwa na visa vya watu na wanyama kutumbukia visimani na kusababisha madhara ikiwemo Ruhuwiko, Boys, Mahenge, na Mjimwema na kusababisha madhara ikiwemo vifo.

Amewataka wananchi kuhakikisha visima vinafunikwa vizuri na kusafishwa na wataalamu ili kuepusha majanga, pia amesisitiza kuwa wananchi wanapokutana na majanga wasijaribu kupambana peke yao kufanya uokozi, bali wawasiliane mapema na Jeshi la Zimamoto ili kusaidia kwa haraka.

SOUWASA imesisitiza kuwa uchimbaji wa visima unaweza kusaidia upatikanaji wa maji, lakini usipofanywa kwa kufuata taratibu unaweza kusababisha magonjwa na hata vifo, hivyo wananchi wanahimizwa kutumia maji ya bomba, kuchimba visima kwa kufuata sheria, na kuhakikisha usalama wa afya na maisha ya jamii.