Mwaka 1995, joto ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) lilikuwa kali. Mchuano wa kuwania tiketi ya chama hicho kwenye mbio za urais ulikaribia kukipasua chama. Jakaya Kikwete, baada ya kuongoza hatua ya tatu bora kwenye Mkutano Mkuu, ilitangazwa yafanyike marudio kwa sababu hakuvuka asilimia 50, wakati Katiba ya chama haikuwa ikisema hivyo.
Kikwete aliongoza dhidi ya Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya. Marudio yalimhusisha Jakaya aliyeongoza ngwe na Mkapa aliyetoka wa pili. Matokeo ya duru ya pili yalibeba ushindi kwa Mkapa.
Baada ya hapo, wana-CCM hasa vijana hawakuridhika. Waliona Kikwete alidhulumiwa ushindi. Timu ya Kikwete, kwa hali ya kuchachamaa, walimshinikiza mwanasiasa huyo kuhama na kujiunga na upinzani. Waliamini Kikwete angehamia chama chochote cha upinzani, angepata fursa ya kugombea urais.
Hata hivyo, Kikwete hakujaa upepo. Aliomba kuzungumza mkutanoni, na hotuba yake ya kukubali kushindwa na kuitaka timu yake imuunge mkono Mkapa, ilisisimua wazee, hasa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais aliyekuwa madarakani wakati huo, Ali Hassan Mwinyi.
Pamoja na Kikwete kukubali kushindwa na kutaka wafuasi wake wote kumuunga mkono Mkapa, wapo watu hawakumwelewa. Waliogoma kumwelewa Kikwete walikuwemo ndani ya wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM hadi nje. Abdul Juma Mluya ni mmoja wa wafuasi walioamini Kikwete alistahili, ambaye hakukubali kurudi nyuma. Alijitoa CCM.
Safari hiyo ya Mluya kuondoka CCM ilianza kituo cha kwanza Chama cha Wananchi (CUF), baadaye Democratic Party (DP), hajawahi kugeuza shingo kurejea alipotoka. Hivi sasa, Mluya ni Mwenyekiti wa DP, pia mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu 2025, akibeba tiketi ya chama hicho.
Mluya aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 1986, wakati huo akiwa na umri wa miaka 12. Alipochukua kadi ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), miaka sita baadaye, yaani mwaka 1992, alikabidhiwa rasmi kadi ya CCM. Mwaka 1995, baada ya kushuhudia Mkapa akipitishwa kuwa mgombea urais dhidi ya Kikwete, aliachana na chama hicho na kujiunga na CUF.
Alikabidhiwa kadi ya uanachama wa CUF mwaka 1996. Ulipofika mwaka 1998, Mluya aliaminiwa na chama hicho na kuteuliwa kuwa mjumbe wa kikosi kazi maalumu kilichoundwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Shaban Mloo (marehemu), kwa ajili ya kuratibu maandalizi ya CUF kushiriki Uchaguzi Mkuu 2000 na kushinda dola.
Pamoja na nafasi hiyo ya kikosi kazi, Mluya aliasisi tawi la Mapambano CUF la Vingunguti, Dar es Salaam. Tawi hilo lilipata usajili namba 8, na kwa mujibu wa Mluya, liliingia kwenye rekodi za CUF kuwa tawi la nane kufunguliwa tangu chama hicho kilipopata usajili wa kudumu Januari 21, 1993.
Mluya alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi la Mapambano CUF, alidumu kwenye nafasi hiyo kwa mwaka mmoja (2000–2001), baada ya hapo alijiweka pembeni lakini akabaki kuwa mlezi wa tawi hilo hadi mwaka 2012, alipoachana na CUF na kujiunga na DP.
Kwa mujibu wa Mluya, mwaka 2012, aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila (marehemu), alimwagiza Ernest Gamba, ambaye wakati huo alikuwa Katibu wa Operesheni wa DP, kumshawishi Mluya kujiunga na DP. Kwa heshima ambayo Mluya alikuwa nayo kwa Mtikila, alikubali. Akakabidhiwa kadi ya uanachama wa DP na Mtikila mwenyewe.
Baada ya kujiunga na DP, Mluya aliteuliwa kuwa Katibu wa Uchumi na Mipango wa chama hicho. Mwaka huo (2012), jimbo la Arumeru Mashariki, Arusha, ulifanyika uchaguzi mdogo wa ubunge baada ya aliyekuwa mbunge wake, Jeremia Sumari, kufariki dunia.
Kwa imani kubwa, licha ya kuwa mgeni kwenye chama, Mluya aliteuliwa kuongoza jopo la kampeni za aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya DP, Mohamed Mohamed. Hata hivyo, Mohamed alitoka wa nne, nyuma ya Joshua Nassari (Chadema) aliyeshinda, Sioi Sumari (CCM) aliyeshika nafasi ya pili na Abdallah Mazengo (AFP). Jumla ya wagombea walikuwa wanane.
Mwaka huohuo, DP ilifanya uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wapya. Mluya aliwania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara. Alishinda na kushikilia nafasi hiyo kwa miaka sita (2012–2018). Mwaka 2018, alipanda ngazi hadi kuwa Katibu Mkuu. Alidumu kwa miaka saba kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti katika uchaguzi uliofanyika Julai 26, 2025.
Karata ya Mluya anapobisha hodi Ikulu ili aingie na kuongoza nchi inaanza na mtaji wa watu wa chini kimaisha. Anasema kuwa siasa zake zinaegemea kwa walalahoi. Ahadi yake ni kwamba atakapochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atajikita kwanza kushughulikia kero za walalahoi ili kuwapa unafuu wa maisha.
Mluya anasema afya ni agenda nyeti na ya msingi kwa sababu mafanikio yoyote ya Serikali yatategemea kwanza afya za wananchi. Anaeleza kwamba afya itakuwa kipaumbele cha kwanza akiwa Rais. Anajenga mtazamo kwamba endapo atafanikisha wananchi kuwa na afya bora, vilevile huduma za afya zikiwa za uhakika na zinazofaa, itamuwia wepesi kufanikisha agenda na vipaumbele vingine.
Mfumo mzuri wa elimu, Mluya anatembea nao kama turufu ya kampeni. Anafafanua kwamba shida haiwezi kuwa elimu, bali mfumo unaotumika kutoa hiyo elimu. Ahadi yake ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo bora wa elimu utakaokomboa kizazi cha Tanzania.
Kilimo na mifugo ni kipaumbele chake kingine. Anasema kilimo ni uti wa mgongo wa taifa. Halafu, anaahidi kudumisha utawala bora unaozingatia Katiba na sheria pamoja na utu wa mtu. Anaapa kupambana na rushwa, pia kujenga miundombinu ya uhakika mikoa yote na kuiunganisha nchi wilaya kwa wilaya, mkoa hadi mkoa.
Mluya anasema kuwa yeye siyo muumini wa Katiba mpya, bali Katiba bora. Anawahakikishia Watanzania kwamba endapo watamchagua kuwa Rais wa Tanzania, ataanzisha mchakato makini utakaowezesha kupatikana kwa Katiba bora itakayoifaa nchi sasa na vizazi vingi vijavyo.
Imani ya Mluya ni kwamba Watanzania wanaoishi ughaibuni (diaspora) ni rasilimali muhimu kwa nchi, lakini haitumiki ipasavyo kwa sababu ya Katiba na sheria zilizopo. Anaeleza kuwa Watanzania waliochukua uraia wa mataifa mengine, wengi wanashindwa kuwekeza Tanzania, ambayo ndiyo nchi yao ya asili, kwa kubanwa na sheria.
Kutibu hilo, Mluya anaahidi akiwa Rais, atahakikisha kunakuwa na mabadiliko ya Katiba na sheria, ili Mtanzania aruhusiwe kuwa na uraia wa nchi zaidi ya moja (uraia pacha). Kwa kufanya hivyo, anaamini Watanzania wa diaspora watakuwa huru kurudi kuwekeza nyumbani, hivyo kuendelea kujenga uchumi wa nchi.
Mambo mengine ambayo Mluya anaahidi kuyawekea mkazo ni mifumo ya kodi, atahakikisha wananchi hawaumizwi na kodi. Kingine, anasema wakandarasi wazawa watapewa kipaumbele kwenye zabuni za Serikali, na pale itakapolazimu kupata mkandarasi wa nje, atapewa sharti la kuingia ubia na mzawa, ili kuhakikisha fedha zinabaki Tanzania.
Mluya ni baba, mwenye mke na watoto watatu wa kiume.
Mkewe jina lake ni Zaitun Kome na watoto ni Juma, Ibrahim na Jamal, ambao wote ni wa kiume.
Mluya alizaliwa Novemba 24, 1974, kwenye kijiji cha Yerayera, kata ya Uyumbu, tarafa ya Usoke, wilayani Urambo, Tabora. Ni mtoto wa kwanza kati ya saba wa familia ya Juma Mrisho Mluya, aliyekuwa Mkuu wa Stesheni ya Treni ya Urambo, na mkewe, Halima Mustafa Komba. Baba wa Mluya alifariki dunia mwaka 1987, mama yake bado yupo hai.
Damu ya siasa inazunguka ndani ya ukoo wa Mluya. Babu yake, Ramadhan Juma Mluya, alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) akitokea Tabora. Mpaka anastaafu siasa, babu huyo alikuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya CCM, Wilaya ya Tabora Vijijini.
Babu mwingine wa Mluya, Ali Juma Mluya, aligombea kura za maoni CCM mwaka 1995, jimbo la Morogoro Mjini, akifanya majaribio ya ubunge. Mdogo wake, Mohamed Juma Mluya, ni Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Vingunguti, Ilala, Dar es Salaam.
Mwaka 1982, Mluya alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Boma, iliyopo Wilaya ya Korogwe, Tanga na kuhitimu darasa la saba mwaka 1988. Alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari Shule ya Ufundi Ifunda, Iringa, kuanzia mwaka 1989 mpaka 1992 alipomaliza kidato cha nne.
Alipomaliza elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo cha Vijana Ihemi Frontline kilichopo Ihemi, Iringa, na kutunukiwa astashahada ya taaluma ya umeme. Pia amesoma kozi fupi za Mafunzo ya Uongozi, vilevile alipokea mafunzo ya Uzalendo wa Nchi na Uongozi kutoka Chuo cha Taifa cha Jeshi (NDC).
Mwaka 2022, Mluya alikuwa mjumbe wa kikosi kazi cha Rais kilichotathmini hali ya kisiasa na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuendesha demokrasia nchini. Vilevile, Mluya alishakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Siasa ya Baraza la Vyama vya Siasa, nafasi hiyo ukomo wake ulikuwa mwaka 2025.