Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame amewapokea madaktari bingwa 30 wa Rais Samia watakaotoa huduma za matibabu kwenye hospitali tano za halmashauri za mkoa.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na matibabu ya magonjwa njia ya uzazi na watoto, huduma za upasuaji wa kibobezi, utoaji wa dawa za usingizi, tiba ya magonjwa ya kawaida, pamoja na kutoa rufaa kwa wagonjwa watakaohitaji matibabu ya kitaalamu katika hospitali za juu.
Akizungumza na madaktari hao Mkuu Makame amewapongeza kwa kujitolea kutoa huduma hiyo, na kuwataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha wanawawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi.
Makame ameeleza kuwa ujio wa kambi hiyo ya madaktari bingwa wa Samia ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya mkoani Songwe.
Amebainisha kuwa, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, mkoa umepata maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la vituo vya afya kutoka 205 hadi 273, na hospitali kutoka mbili hadi tano vyote kwa lengo la kuboresha huduma za msingi na za kitaalamu kwa wananchi.
“Serikali imetenga zaidi ya Sh40.6 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu, ununuzi wa dawa, vifaa, na vitendanishi, pamoja na kuanzisha afua mbalimbali za tiba ikiwemo lishe, kudhibiti malaria, Kifua Kikuu na Ukimwi.
“Kupitia juhudi hizi, upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa asilimia 90, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 320 mwaka 2022 hadi 146 mwaka 2023, mkoa umepokea watumishi wa sekta ya afya 725 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi wa afya, na kufanya huduma kuwa za karibu zaidi kwa wananchi,” amesema Makame.
Amewataka viongozi na watendaji wa mkoa kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa karibu kwa madaktari ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinafikia viwango vya juu, na wananchi wanafaidika kwa kiwango cha juu.
Kwa upande wake Mratibu wa huduma hiyo kutoka Wizara ya Afya, Pasclina Andrew amesema kuwa uwekezaji huo mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya ni hatua muhimu katika kuimarisha afya ya wananchi wa Songwe na kuboresha huduma za matibabu, kwani sasa wananchi hawatalazimika kusafiri kwenda mikoa jirani kwa huduma za kibingwa.
“Pia, kambi hii itaimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa kitaalamu (mentorship), na kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi mkoani hapa,” amesema Pasclina.
Timu ya madaktari hao 30 wanatarajia kutoa huduma mkoba kwa muda wa wiki moja katika halmashauri tano za mkoa huo.