Tanzania inajiandaa kuandika historia ya kuwa mwenyeji wa mbio za magari za ubingwa wa Afrika 2025, Mkwawa Rally of Tanzania, zitakazofanyika kuanzia Septemba 19 hadi 21 mkoani Morogoro.
Zaidi ya madereva 23 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo yatakayohusisha jumla ya kilometa 338.
Mashindano haya yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali, hasa kati ya anayetabiriwa ubingwa Mtanzania, Yasin Nasser akisaidiwa na Ali Katumba, anayeshika nafasi ya kwanza akiwa na alama 116, na mpinzani wake kutoka Kenya, Samman Singh Volhra akishirikiana na Drew Sturrock kutoka Uingereza mwenye alama 106.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana Septemba 15.2025 mjini hapa, Mkuu wa Habari wa Mashindano ya Magari Tanzania, Mike Maluwe, alisema Nasser ana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa endapo ataibuka mshindi na kupata alama 30.
“Endapo Nasser atamaliza wa kwanza, ataweka historia kwa kuwa bingwa wa Afrika 2025, lakini atakumbana na changamoto kubwa kutoka kwa Samman Singh na Ahmed Huwel,” alisema Maluwe.
Aliongeza dereva wa Tanzania, Ahmed Huwel akisaidiwa na Viljem Oslaj kutoka Slovenia anatarajiwa kutoa upinzani mkubwa baada ya kuingia na gari jipya aina ya Toyota Yaris Rally 2.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mashindano hayo, Satinder Birdi, alisema Tanzania inanufaika kwa kuwa mwenyeji wa mzunguko wa mwisho wa mbio hizo ambapo bingwa atapatikana nchini Tanzania
Alisema mbali na washiriki kutoka Afrika Mashariki, pia madereva kutoka India watashiriki huku Watanzania wakipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
Kutoka Tanzania, madereva wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na Altaaf Munge akisaidiwa na Victor Jackson, Shrhzad Munge na Aaron John, pamoja na Prince Charles Nyerere.
Aidha, kuna kundi la madereva 12 wa ndani wanaotarajiwa kushindana kugombea kombe la kitaifa.
Msimamizi wa mbio hizo, Dk. Mosi Makau, alisema mashindano yataanza Septemba 19 eneo la Tungi, mashamba ya mkonge, na kuendelea Septemba 20 na 21 katika shamba la msitu la Mkundi TFS.
Kwa siku tatu, madereva watakimbia umbali wa kilometa 338, kila hatua ikihusisha mizunguko miwili miwili.
Wadhamini wakuu wa mashindano haya ni Mkwawa Group of Companies, kupitia Afisa Fedha Emmanuel Mhagama, ambaye alisema wamejipanga kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha maandalizi na usalama vinakuwa bora.
Alisema magari ya dharura, askari polisi, vikosi vya FFU na zimamoto vitakuwepo kuhakikisha mashindano yanafanyika salama kwa madereva na mashabiki.