Mwanza. Masista wanne wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, wamefariki dunia baada ya gari lao kugongana uso kwa uso na lori mkoani Mwanza.
Waliofariki ni pamoja na Mama Mkuu wa Shirika hilo duniani, Sista Nelina Semeoni (60), raia wa Italia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 15, 2025 saa 1:50 usiku katika kijiji cha Bukumbi, Kata ya Idetemya, Wilaya ya Misungwi, barabara ya Usagara-Kigongo Feri.
Masista hao walikuwa wakielekea uwanja wa ndege wa Mwanza wakitokea Jumuiya ya Bukumbi, wilayani Misungwi.
Mbali na Sista Nelina, pia waliopoteza maisha ni msaidizi wake, Sista Lilian Kapongo (55), mkazi wa Tabora, Sista Damaris Matheka (51), Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi na raia wa Kenya pamoja na Sista Stellamaris Muthin (48), raia wa Kenya pia na dereva wa gari walilokuwa wakisafiria, Boniphace Msonola (53).
Sista Pauline Mipata (20), Msimamizi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi, amenusurika kifo katika ajali hiyo na amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu.
Kabla ya ajali hiyo, masista hao walikuwepo mjini Kahama, mkoani Shinyanga kwa ajili ya sherehe ya Nadhiri za Daima za masista wenzao watatu, zilizoadhimishwa Jumamosi Septemba 13, 2025 katika Jimbo Kuu Katoliki la Kahama.
Sherehe hiyo ndiyo hatua ya mwisho kwa masista kujiweka rasmi katika maisha ya utawa wa kudumu.
Baada ya sherehe, walielekea Mwanza kwa maandalizi ya safari ya kwenda Dar es Salaam ambapo wakiwa njiani walipata ajali.
Taarifa ya Mutafungwa iliyotolewa leo Jumanne Septemba 16, 2025 imeeleza kuwa gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi lilihama njia, hivyo kutokea ajali hiyo.
Gari hilo lililoendeshwa na Boniphace Msonola (marehemu) lilihama upande wa kulia wa barabara na kugongana uso kwa uso na lori aina ya Sino Truck, mali ya Kampuni ya Nyanza Road Works, lililokuwa linaendeshwa na Venance Mashaka (61), mkazi wa Buhongwa.
“Katika ajali hiyo watu wanne walifariki katika eneo la ajali na mmoja ambaye alikuwa akiendesha Land Cruiser alifariki katika Hospitali ya Bukumbi wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
“Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari ndogo kwa kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari kisha kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa linakuja mbele kwa mbele,” amesema Mutafungwa.
Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi wa kitabibu, huku dereva wa lori akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.
Jeshi la Polisi limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendokasi na kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara.