Ahadi za Mwinyi kwa bodaboda, wakulima na wajasiriamali

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amesema akipata ridhaa nyingine ya kuongoza, watawekeza nguvu kubwa kuyainua makundi ya wajasiriamali, huku bodaboda wakiundiwa ushirika wa kumiliki pikipiki zao wenyewe.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Septemba 16, 2025, wakati akizungumza na makundi ya bodaboda, wakulima wa viungo na wajasiriamali katika eneo la Mndo Dole, Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya kampeni na kuomba kura katika makundi hayo.

Amesema iwapo wakipewa fursa nyingine, Serikali itatenga maeneo maalumu kwa ajili ya kilimo.


“Sio tu itatoa maeneo, bali pia itatoa pembejeo, vitendea kazi, mbolea, mbegu na kuwatafuta masoko ya uhakika ili kilimo chao kiwe na tija,” amesema.

Mbali na hayo, amesema pia Serikali itatoa mitaji ya biashara ili wajasiriamali wapate mambo hayo. “Tunayasema haya tukitambua tuna uwezo wa kuyatekeleza, na hilo halina shaka kwani tulioahidi mwaka 2020 mmeona wenyewe tulivyotekeleza kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Amesema Serikali imeanzisha Wakala wa Kuwezesha Wananchi Kiuchumi (ZEEA) ambao utasimamia wajasiriamali na kutoa mikopo, na bapo kwa kipindi cha miaka mitano wametoa mikopo zaidi ya Sh90 bilioni.

“Tukirejea madarakani, mikopo hiyo itaongezwa zaidi ili wengi wanufaike,” amesema mgombea huyo.

Dk Mwinyi amesema mipango yao imejikita katika maeneo matatu makuu ambayo ni kumaliza changamoto ya ajira, kutoa ajira serikalini na katika sekta binafsi, na kuwawezesha wananchi kiuchumi, ambalo ndio eneo kubwa linalochukua ajira nyingi.

Amesema watashahihisha sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi ili kujenga viwanda, ambapo michakato hiyo imeshaanza na wametenga maeneo maalumu ya kujega viwanda, kwa Unguja ni Dunga Zuze na Pemba ni Micheweni.


“Eneo lingine ni kuwawezesha vijana kujiajiri, na hapa ndio tutatoa mikopo na kurahisisha upatikanaji wa vifaa kulingana na sekta husika,” amesema Dk Mwinyi.

Akizungumza kuhusu bodaboda, amesema lengo lake ni kuwa na ushirika na wajasiriamali wenyewe kwa bodaboda wanazozimiliki, badala ya kutumia bodaboda za watu wengine.

Awali, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, ameeleza changamoto za makundi hayo, akisema iwapo chama kitapata ridhaa nyingine, kitahakikisha kinasimamia Serikali kushughulikia matatizo yao.

Amesema amepitia kwenye makundi hayo na kuzungumza nayo, na kubaini matatizo licha ya mafanikio kadhaa ambayo yaliyopatikana.

Kwa upande wa wajasiriamali, amesema wanakosa vitambulisho vya ubora wa bidhaa zao na kukosa fursa za mikopo kwa baadhi yao.

Kuhusu wakulima wa viungo, amesema wanakosa miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo, na kukosa soko la ndani na nje.

“Uwezeshaji mdogo, uhaba wa wataalamu, masharti magumu na mlolongo mrefu wa kupata ithibati na vitambulisho kutoka kwa taasisi zinazohusika,” amesema Dk Dimwa.

Awali, mgombea uwakilishi Bububu, Ramadhani Soraga, amesema katika eneo la kilimo cha viungo wametoa mafunzo bure kwa vijana zaidi ya 400 na kupatiwa cheti, ambapo kwa kawaida mafunzo hayo yanalipiwa Dola 800 za Marekani.

“Kwa maagizo yako tumetoa bure na tunaendeleza kutoa mafunzo kwa waendesha watalii ili kufanikisha uwezeshaji wao,” amesema.