Dar es Salaam. Wabebaji walitumia dakika sita kukamilisha kuyaingiza majeneza yote ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama na dakika 32 baadaye ibada ya faraja ilianza ikiongozwa na Mchungaji wa kanisa hilo, Eliona Kimaro.
Akisoma wasifu wa marehemu kanisa hapo, msemaji wa familia amesema Francis Elineema Kaggi ameacha mke na mtoto mmoja, Michelle.
Amesema, Francis alifunga ndoa na Sophia Charles Makange mwaka 2002 na kubahatika kupata watoto wanne.
“Enzi za uhai wake alifanya kazi katika taasisi mbalimbali na kuajiriwa Shirika la Ugavi la Umeme Tanzania (Tanesco) kama Ofisa mkuu wa Tehama hadi mauti ilipomkuta.
Akiwaelezea wengine waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo, amemtaja binti mkubwa wa Francis, Janemary (2001), ambaye hadi anafariki alikuwa Ofisa Biashara na Viwanda wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Tabora.
Mwingine ni binti wa pili wa Francis, Maria (2005) ambaye alihitimu kidato cha sita mwaka huu na kijana wa mwisho, Joshua (2018) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sunrise, sanjari na ndugu yao mwingine, Elineema Hamis Kaggi (1990) ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa Mhasibu wa Tanesco makao makuu.
Imeelezwa, marehemu hao walipata ajali ya gari wakirejea Dar es Salaam kutokea Tanga ambako walikwenda kwenye mazishi ya mama mzazi wa marehemu Francis.
Watu watano kati ya saba waliokuwa kwenye gari iliyoibeba familia hiyo walipoteza maisha, miongoni mwa walionusurika katika ajali hiyo ni mke wa marehemu, Sophia ambaye ni Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisutu Dar es Salaam. ambaye leo amewaongoza waombolezaji kuaga miili ya wapendwa wake akipewa usaidizi wa kushikiliwa na waombolezaji wengine.
Endelea kufuatilia Mwananchi.