Arusha. Usimamizi mbovu wa mikataba ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri imetajwa kama kaa la moto, linaloteketeza mabilioni ya fedha za Serikali.
Kutokana na hilo, Serikali imewataka wataalamu wa sekta ya ujenzi na usafirishaji kuhakikisha wanaongeza uelewa, umakini na kuweka uwazi katika mikataba ya miradi ya miundombinu, ili kulinda thamani ya fedha za umma.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Florian Kabaka wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya usimamizi wa mikataba ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri iliyoshirikisha wahandisi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Kabaka amesema kuwa miradi mingi ya miundombinu ya usafiri imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi za kucheleweshwa, kuzidi bajeti au kushindwa kufikia viwango vya ubora kutokana na udhaifu wa mikataba na usimamizi.
Akitolea mfano Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024, Kabaka amesema kuwa ilibaini upotevu mkubwa wa fedha za umma kupitia miradi iliyosimamiwa vibaya.
“Mfano Tanroad (Wakala wa Barabara Tanzania) ilipoteza zaidi ya Sh579 milioni kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya fomula ya kurekebisha bei, huku mradi wa maji taka Babati ukisababisha malipo ya ziada ya Sh1.6 bilioni kwa kazi ambazo hazikupangwa,” amesema na kuongeza;
“Ripoti hiyo pia inaonyesha miradi mingine iligharimu Serikali zaidi ya bajeti ya awali, mfano fidia ya mradi wa bwawa la Kidunda ilipanda kutoka Sh3.8 bilioni hadi Sh9.07 bilioni ambalo ni ongezeko la takribani Sh5.24 bilioni.”
Vilevile, upungufu wa usanifu katika Soko la Mwanza ambapo Kabaka amesema uliongeza Sh1.96 bilioni, huku Soko la Kariakoo likihitaji Sh757 milioni zaidi kutokana na tafiti hafifu.
“CAG pia alibaini visa vya ufisadi na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, ikiwemo mikataba 251 yenye thamani ya Sh13.45 bilioni kusainiwa bila uhakiki wa kisheria, Vilevile, Sh2.01 bilioni zililipwa taslimu badala ya kupitia benki, hali iliyoongeza mianya ya matumizi mabaya ya fedha.”
Akiangazia ucheleweshaji wa miradi na ubora hafifu, Kabaka amesema kuwa miradi mingi imekuwa ikicheleweshwa kwa muda mrefu, huku mingine ikiharibika mapema kutokana na vifaa duni.

“Mfano ni mradi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga wenye thamani ya Sh449 bilioni, ambao ulicheleweshwa kwa zaidi ya miezi 28 kutokana na changamoto za kifedha kati ya Serikali na Benki ya Uwekezaji,” amesema na kuongeza;
“Mifano hii yote na mingine mingi inaonyesha changamoto halisi zinazohitaji suluhu za dharura na za vitendo, hivyo nawaomba mchukulie siku hizi tano kama fursa ya kutoa suluhu za kweli ya kila shilingi ya umma inayotumika lazima ilete matokeo yanayoonekana na kudumu.”
Pia amewataka wataalamu hao kuhakikisha katika mijadala yao wanalenga kuimarisha usimamizi wa mikataba, kutekeleza uwajibikaji na uwazi, kuondoa upotevu na ufisadi.
“Miundombinu ya barabara, bandari na usafiri wa anga ni uti wa mgongo wa uchumi na ustawi wa kijamii, ikirahisisha kilimo, biashara, afya, elimu na huduma nyingine muhimu na Serikali imewaamini ninyi, leteni mbinu bunifu zitakazosaidia kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi,” ameagiza.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wataalamu wa Barabara Tanzania (Tara) yamewakutanisha wahandisi 62 kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Mjumbe wa bodi wa Tara, Abdul Awadh amesema kuwa mafunzo hayo ya siku tano (kuanzia Septemba 15, 2025 hadi 19) ya usimamizi wa mikataba ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri yameandaliwa kwa kuzingatia viwango bora vya Kimataifa, kama vile vilivyotengenezwa na Shirikisho la Kimataifa la Wahandisi Washauri (FIDIC).

Amesema kuwa katika mafunzo hayo yatakayotolewa na wataalamu wabobezi kutoka Tanzania, Zambia na Ethiopia zitalenga kujenga uelewa juu ya usimamizi bora wa mikataba ili kuhakikisha ubora, uwajibikaji, thamani ya fedha na uendelevu wa muda mrefu.
“Siku hizi tano pia tutajengeana uwezo wa jinsi ya kuchambua kesi, mada kuhusu mbinu za zabuni, mifumo ya utekelezaji wa mikataba, usimamizi wa madai, utatuzi wa migogoro, mabadiliko ya mikataba na tutakuwa na masomo kwa vitendo,” amesema.
Amesema lengo ni kusaidia Serikali kuepuka hasara zinazopatikana kutokana na sekta hiyo.
Naye Mkuu wa kitengo cha mahusiano Tarura, Catherine Sungura amesema mafunzo hayo yanasaidia uelewa katika utekelezaji wa miundo mbinu yao ya barabara.
“Kwa sasa tunatekeleza miradi ya barabara yenye zaidi ya kilomita 1,044 ambayo bila kuongeza uelewa tunaweza kujikuta tunasaini mikataba yenye kuleta hasara kwa Serikali,” amesema Sungura.